Man United yamvizia Watkins
Manchester United wameanzisha tena mawasiliano na Aston Villa juu ya uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wao tegemeo, Ollie Watkins, ikiwa ni sehemu ya jitihada mpya za kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kabla ya msimu mpya kuanza.
Kwa mujibu wa The Telegraph, Villa wamesisitiza kuwa Watkins hauzwi, ingawa wanaonekana kushikilia msimamo wa kutopokea ofa yoyote isiyofikia kiwango cha pauni milioni 60 (Sh208 bilioni). Mkataba wa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England unamalizika mwaka 2028.
United walipata wakati mgumu msimu uliopita katika safu ya ushambuliaji, huku Rasmus Højlund na Joshua Zirkzee wakikosa kasi ya mabao iliyotarajiwa. Kocha Ruben Amorim tayari ametumia kiasi kikubwa kwenye safu hiyo, akimsajili Matheus Cunha kwa paundi milioni 62.5 na Bryan Mbeumo kwa paundi milioni 65 ikiwa ni jumla ya Sh441 bilioni.
Watkins, mwenye umri wa miaka 29, amefunga jumla ya mabao 87 akiwa na Aston Villa yakiwemo 75 ya Ligi Kuu katika misimu mitano, akiwa na wastani wa mabao 15 kwa msimu. Hii inamfanya kuwa chaguo la kuvutia kwa United wanaotaka mshambuliaji mwenye uzoefu wa kutosha katika EPL.
Hatima ya Rashford yafungua mlango
Hatua ya Marcus Rashford kuhamia kwa mkopo Barcelona, ambako kutakuwa na kipengele cha kumnunua kwa paundi milioni 40 (Sh139 bilioni) inamaanisha United watahitaji mshambuliaji mwingine na Watkins anaonekana kama chaguo linalopendelewa.
Hata hivyo, United hawajatoa ofa rasmi kwa Villa hadi sasa. Hatua yoyote kubwa itategemea uwezo wao wa kuuza baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza ili kujiimarisha kifedha.
Afya imara yamvutia Amorim
Mojawapo ya sifa zinazowavutia United kwa Watkins ni historia yake nzuri ya kutokuwepo majeruhi ya muda mrefu. Mshambuliaji huyo amecheza mechi zote za Premier League akiwa Aston Villa msimu uliopita na ameonekana kwenye mechi 184 kati ya mechi 190 za ligi tangu ajiunge. Kwa klabu kama United ambayo imekuwa ikikumbwa na majeruhi mara kwa mara, hii ni faida isiyopaswa kupuuzwa.
Iwapo United wataendelea na mpango huu, itakuwa ni mabadiliko ya mkakati wa uongozi wa Sir Jim Ratcliffe, ambaye amekuwa akilenga zaidi wachezaji vijana wa kuwekeza kwa muda mrefu. Watkins atatimiza miaka 30 mwaka huu lakini inaelezwa kuwa Ruben Amorim anapendelea wachezaji waliokomaa tayari kwa mafanikio ya haraka.
Kwa upande wake mshambuliaji Højlund ameweka wazi kuwa hana mpango wa kuondoka United licha ya tetesi.
“Nina mkataba hadi 2028, hivyo natarajia kusalia Manchester United, najua kuna maneno mengi huko nje, lakini ukweli ni kuwa mimi ni mchezaji wa Manchester United. Nipo tayari kwa pre-season na msimu mpya,” alisema mwezi Juni.