Mbeumo kukipiga Old Trafford msimu ujao
Muktasari:
- United wanajiandaa kumpeleka Mbeumo kwenye ziara yao ya maandalizi Marekani, ambako ataanza maisha mapya akiwa chini ya Amorim na kikosi chake kipya kuelekea msimu mpya wenye matarajio makubwa.
Hatimaye Manchester United wamefanikiwa kumsajili Bryan Mbeumo kwa dau la pauni milioni 71 (Sh249 bilioni) lakini taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo bado haijaridhishwa na namna Brentford walivyoshughulikia mazungumzo ya uhamisho huo.
Mbeumo, mshambuliaji raia wa Cameroon mwenye umri wa miaka 25, ametia saini mkataba wa miaka mitano na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi. United italipa pauni milioni 65 (Sh228 bilioni) kama ada ya msingi, huku pauni milioni 6 zikiwa kama nyongeza kulingana na mafanikio ya mchezaji huyo.
Akizungumza baada ya kutambulishwa rasmi, Mbeumo amesema: "Mara tu niliposikia kuna uwezekano wa kujiunga na Manchester United, sikuweza kufikiria mara mbili. Ni klabu ya ndoto zangu, timu niliyokuwa navaa jezi yao nikiwa mdogo.
"Nina njaa ya mafanikio. Kila siku nataka kuwa bora kuliko jana. Najua nina moyo na nidhamu ya kufikia viwango vingine vikubwa hapa, nikiwa chini ya kocha Ruben Amorim na nikiwa na wachezaji wa daraja la juu.
"Nimesikia mengi kuhusu mazingira mazuri yaliyopo hapa, mipango mikubwa ya baadaye, na mashabiki wa kipekee. Klabu hii ni kubwa, ina uwanja wa ajabu na mashabiki wa aina yake. Tumejipanga kuwania makombe makubwa," amesema Mbeumo.
Licha ya furaha ya kufanikisha dili hilo, taarifa kutoka ndani ya United zinaeleza kuwa viongozi wa klabu hiyo wamekasirishwa na mbinu za Brentford ambao waliongeza bei ya mchezaji hadi kufikia pauni milioni 77 na kumwekea presha Mbeumo kupunguza mishahara yake ili afanikishe uhamisho kwenda Old Trafford au abadili uelekeo na kukubali kujiunga na Tottenham.
Kwa upande wao, Brentford nao hawakuridhishwa na ofa za awali za United ya pauni milioni 55 (Sh193 bilioni) na baadaye milioni 62.5 (Sh217 bilioni) ambazo waliziona kuwa chini ya ile ya Tottenham, huku United wakiwa wanamshawishi mchezaji kwa masharti mazuri binafsi.
Pamoja na sintofahamu hizo, Manchester United wanafurahia kufanikisha usajili wao wa pili mkubwa wa dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kumchukua Matheus Cunha kutoka Wolves kwa pauni milioni 62.5. Viongozi wa klabu wanaamini hilo ni uthibitisho wa sera yao mpya ya mpira kwanza kuanza kuzaa matunda, na kwamba jina lao bado lina mvuto mkubwa kwa nyota wakubwa duniani.
Mkurugenzi wa mpira wa miguu wa United, Jason Wilcox, amesema: “Rekodi ya Bryan katika mabao na pasi za mwisho kwenye EPL ni ya kuvutia. Amedumu kwa misimu mitatu akiwa miongoni mwa wachezaji tija zaidi nchini. Alivyoamini katika mradi wetu na kuonyesha nia ya dhati kujiunga nasi, ilithibitisha kwamba yeye ndiye mtu sahihi kwa ajili ya mpango tunaoujenga. Tumejivunia kufanikisha usajili huu kabla ya kuanza ziara ya Marekani.”
Kwa sasa, United wanajiandaa kumpeleka Mbeumo kwenye ziara yao ya maandalizi Marekani, ambako ataanza maisha mapya akiwa chini ya Amorim na kikosi chake kipya kuelekea msimu mpya wenye matarajio makubwa.