Kisa Barcelona, Rashford apunguza mshahara
Muktasari:
- Rashford anasubiri kuidhinishwa na La Liga ili aweze kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshiriki msimu ujao wa mashindano.
Barcelona, Hispania. Nyota wa zamani wa Manchester United, Marcus Rashford, ameonekana mjini Barcelona usiku jana Jumapili, huku ikithibitishwa kuwa amejiunga na miamba hiyo ya Catalonia kwa mkopo baada ya kukubali kupunguzwa mshahara kwa asilimia 15 ili kufanikisha ndoto yake ya kucheza katika klabu hiyo ya Hispania.
Rashford, ambaye alikuwa amepoteza nafasi yake kikosini Old Trafford chini ya kocha Ruben Amorim, amekuwa chaguo la kwanza kwa Barcelona msimu huu wa joto licha ya klabu hiyo kuonesha nia pia kwa nyota wa Liverpool Luis Díaz na winga wa Hispania, Nico Williams.
Barcelona, ambao wanakabiliwa na matatizo ya kifedha kwa muda mrefu, bado hawajafanikiwa kumsajili rasmi Rashford katika orodha ya wachezaji wa La Liga kutokana na vikwazo vya usajili. Hata hivyo, kukubali kwake kupunguziwa mshahara kutoka Sh1 bilioni kwa wiki hadi chini ya hapo kunaongeza uwezekano wa kusajiliwa mapema, pengine baada ya ziara ya maandalizi barani Asia.
Taarifa zinasema Rashford hana kipengele cha kununuliwa moja kwa moja mwishoni mwa mkopo wake, lakini tayari ameshatangaza wazi kuwa anatamani kucheza na kinda Lamine Yamal.
Mshambuliaji huyo aliyetua Nou Camp kwa ndege binafsi, anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya leo (Jumatatu) na kuanza mazoezi rasmi Jumanne.
Katika klabu hiyo, Rashford anatarajiwa kuchagua kati ya jezi namba 14, 19 au 22 ambazo ziko wazi kwa sasa. Namba 14 ni ya kihistoria, ikiwa ilivaliwa na gwiji Johan Cruyff na pia mchezaji aliyekuwa shujaa wa Rashford, Thierry Henry.
Namba 19 iliachwa na Lamine Yamal aliyekabidhiwa namba 10 hivi karibuni, jezi ambayo pia iliwahi kuvaliwa na Lionel Messi.
Aliyekuwa mchezaji mwenzake Rashford pale Manchester United, Paul Pogba, ametoa pongezi kwa uhamisho huo.
"Ni jambo kubwa, lakini nafurahi kwa ajili yake kwa sababu walimnyang’anya namba yake. United wamepoteza mchezaji mkubwa. Ni bahati mbaya kwao, lakini ni dili nzuri sana kwa Barcelona," amesema Pogba.
Rashford alikuwa akivaa jezi namba 10 United kabla ya kukabidhiwa Matheus Cunha, aliyesajiliwa kutoka Wolves kwa dau la pauni milioni 62.5.
Kwa sasa, Rashford anasubiri kuidhinishwa rasmi na La Liga ili aweze kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshiriki msimu ujao wa mashindano.