Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema, CCM wanavyotikisa anga za kisiasa



Dar es Salaam. Ziara za kisiasa zinazoendelea kufanywa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mikoa mbalimbali nchini zimeibua ushindani wa kisiasa, huku viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakifuata nyayo zao katika maeneo hayo kwa lengo la kujibu na kufafanua hoja zinazotolewa na wapinzani.

Mbali na CCM, baadhi ya viongozi wa Serikali pia wamejikuta wakitoa ufafanuzi kuhusu masuala yanayoibuliwa na viongozi wa upinzani, hali inayochangia kuongezeka kwa mjadala na joto la kisiasa nchini.

Kwa sasa, viongozi wa Chadema wameenea katika mikoa mbalimbali wakitekeleza Operesheni Free Tundu Lissu na Katiba Mpya, wakihamasisha wananchi kuhusu madai ya mageuzi ya kisiasa na mabadiliko ya Katiba.

Ujumbe wa Chadema unaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche, ukijumuisha wajumbe wa Kamati Kuu akiwemo Godbless Lema, Mwenyekiti wa Kanda ya Mashariki, Boniface Jacob, pamoja na viongozi wa jumuiya za chama hicho, ikiwemo Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).

Kwa upande wa CCM, viongozi wake wamegawanyika katika makundi tofauti yanayofanya ziara katika maeneo ambayo Chadema imekwishapita.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi ametembelea mikoa ya Singida, Iringa na baadhi ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na viongozi wa upinzani waliopita huko.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Ally Hapi, amekuwa akifanya ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, akieleza sera, mafanikio ya Serikali na kujibu hoja zinazotolewa na wapinzani katika ukanda huo.

Mwenendo huo wa viongozi wa vyama vikuu vya siasa kufuatana katika maeneo yale yale unaonyesha ushindani unaozidi kushika kasi, huku kila upande ukitumia mikutano ya hadhara kuwasilisha hoja zake na kushawishi wananchi kuunga mkono ajenda zake za kisiasa.

Julai 1, 2026 Kihongosi anatarajiwa kuanza ziara katika Mkoa wa Pwani, ambako tayari Chadema ilishapita, huku Hapi naye akitarajia kuanza ziara katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Mbeya na Kusini, ambako pia Chadema imeshapita.


Si jambo la ajabu

Kinachoshuhudiwa katika ziara hizo kimeelezwa na Dk Hamis Mwalyosi, mchambuzi wa Siasa kuwa si cha ajabu katika mfumo wa siasa za vyama vingi, kwani kazi ya chama tawala ni kutetea sera na utekelezaji wa Serikali, huku upinzani ukiwa na jukumu la kuhoji, kukosoa na kushinikiza maboresho.

Alisema tofauti iliyopo sasa ni kwamba mijadala hiyo imehamia zaidi kwenye mikutano ya hadhara na majukwaa ya kisiasa, badala ya kubaki bungeni, kwa kuwa upinzani hauna uwakilishi wa kutosha katika Bunge.

Aligusia hoja ya Katiba Mpya, akisema imekuwa sababu ya mvutano kila upande unataka kuonekana kuwa ndiye mwenye dhamira ya kweli ya kuifikisha nchi huko.

Alisema wakati Chadema inataka kuonyesha kuwa ndiyo mwenye ajenda ta Katiba mpya, CCM nayo inajenga hoja kwamba suala hilo tayari limo ndani ya mipango yake rasmi ya kisiasa kupitia ilani ya uchaguzi.

“Muhimu si nani anadai Katiba mpya, bali ni nani anaweza kuonyesha njia ya kuifikia. Wananchi watapima zaidi matokeo kuliko kauli za kisiasa,” alisema.

Hata hivyo, Mchambuzi wa siasa, Profesa Besela Balama, yeye anaona kasi ya majibizano ya kisiasa inayoshuhudiwa inaonyesha kuamka kwa siasa za ushindani.

“Demokrasia yenye afya inahitaji hoja zikabiliane kwa hoja. Tatizo hujitokeza pale ambapo mjadala unahamia kwenye mashambulizi binafsi badala ya kujikita katika takwimu, sera na ushahidi. Wananchi wanahitaji majibu ya changamoto zao, si mashindano ya nani ana sauti kubwa zaidi,” alisema.


Hoja zinazotikisa

Mbali na shinikizo la Chadema la kutaka mwenyekiti wake, Tundu Lissu, anayeshikiliwa gerezani akikabiliwa na mashtaka ya uhaini aachiwe huru bila masharti, suala jingine linalotawala ziara hizo ni madai ya kupatikana kwa Katiba Mpya.

Juni 17, mwaka huu, akiwa jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, aliitaka Serikali kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya maandalizi ya mchakato wa uandishi wa Katiba Mpya. Wakati huohuo, alitangaza kuwa chama hicho kimeunda kamati ya watu 11 itakayoratibu maandalizi ya rasimu ya Katiba.

Kwa mujibu wa Mnyika, hatua hiyo inalenga kuharakisha maandalizi ya mchakato huo na kuonyesha dhamira ya chama katika kushirikisha wadau mbalimbali bila kutegemea matumizi makubwa ya fedha za umma.

Mbali na Mnyika, madai ya Katiba Mpya yamekuwa sehemu ya ujumbe wa viongozi wa Chadema katika ziara zao mbalimbali, huku wananchi wakichangia fedha za kuendeleza harakati hizo kupitia kampeni maarufu ya “Tone Tone”.

Pamoja na viongozi wa CCM wanaoyazungumzia kila mara, madai hayo ya Katiba yalijibiwa Juni 23, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipokuwa akijibu hoja mbalimbali bungeni jijini Dodoma.

Katika majibu yake, Profesa Mkumbo alisema CCM ndicho chenye uhalali wa kuzungumzia suala la Katiba mpya kwa kuwa limejumuishwa katika Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030.

“Watu wanaenda kule wanafanya maandamano na mikutano ya kudai Katiba mpya, CCM tayari ilishaahidi Katiba mpya kwenye Ilani yake,” alisema.

Aliwataka wananchi kutopotoshwa na yeyote anayejifanya kuwa na ajenda kubwa zaidi kuhusu Katiba mpya kuliko chama kilichoiweka kwenye ilani yake.

Chadema ambayo haikushiriki uchaguzo mkuu wa mwaka 2025 ikishinikiza mabadiliko kwenye Katiba na mifumo ya uchaguzi, imekuwa na ajenda hiyo kwa muda mrefu, na kila mara imekuwa ikitumia ziara zake mikoani ikisisitiza suala hilo.

Katikati ya shinikizo hilo, tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, amekuwa akieleza mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa suala hilo kisha kulizogeza mbele kwa sababu mbalimbali.

Alipounda kikosi kazi cha kumshauri kuhusu suala hilo na mengineyo, kilikuja na majibu kuwa Katiba ije baada ya uchaguzi wa mwaka 2025 huku Tume ya kuchunguzua matukio ya vurugu baada ya uchaguzi huo, ilishauri Katiba ipatikane mwaka 2028 ili itumike katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2029 na uchaguzi mkuu 2030.

Vijembe vya kisiasa

Ukiacha suala la Katiba mpya, vijembe vya kisiasa vimekuwa vya kawaida katika kipindi hiki baina ya makada wa pande hizo mbili.

Mathalan, Juni 13 mwaka huu, Kihongosi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa ana taarifa za baadhi ya viongozi wa Chadema kupanga maandamano na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Aliwataka Watanzania kupuuza wito wowote wa maandamano na kusisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila utulivu wa kisiasa.

Haikuchukua muda, siku iliyofuata, Msemaji wa Chadema, Brenda Rupia, Makamu mwenyekiti wa Chadema John Heche na Mnyika kwa nyakati tofauti waalimjibu Kihongosi, wakisema CCM imeshindwa kuthibitisha tuhuma hizo na kwamba madai hayo ni sehemu ya propaganda za kisiasa zinazolenga kuichafua Chadema mbele ya wananchi.

Wakati Rupia alitaka waliotajwa kuwa wanalipwa kuandaa vurugu watajwe hadharani na ushahidi kutolewa, Heche na Mnyika walisema Kihongosi anapotosha suala la wafadhili wa chama hicho kutoka nje ya nchi, wakimtaka kama anataka uwazi naye aweke wazi pia wafadhili wa chama chake kutoka pia nje.


Hapi vs Heche

Akiwa ziarani Shinyanga Juni 5, mwaka huu, Hapi, aliwataka viongozi wa Chadema kuelekeza nguvu zao katika kuwasilisha sera na mipango ya maendeleo badala ya kuendelea na alichokiita malalamiko ya kisiasa.

Alisema wananchi wanahitaji kusikia suluhisho la changamoto za maisha yao kuliko mijadala ya kisiasa isiyoisha.

Hoja hiyo ilijibiwa siku hiyohiyo na Heche, akiwa ziarani na viongozi wengine wa chama hicho katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwa CCM imekuwa ikikwepa kujibu hoja za msingi zinazohusu mabadiliko ya kisiasa kwa kuzitafsiri kama malalamiko.

Alisema kazi ya chama cha upinzani ni kuhoji, kukosoa na kusukuma maboresho pale kinapoona kuna mapungufu katika uendeshaji wa nchi.


Hoja ya mikopo

Akiwa mkoani Ruvuma katika ziara za chama hicho, Heche aliibua hoja kuhusu changamoto zinazoendelea kuyakabili maeneo mbalimbali nchini, licha ya Serikali kuendelea kukopa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kutokana na hali hiyo, alihoji mikopo hiyo inatumika wapi, akitilia shaka kuwa huenda fedha zinazokopwa hazitumiki ipasavyo na ndiyo maana maendeleo yanachelewa kuonekana katika baadhi ya maeneo.

Hoja ya Heche ilijibiwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliyesema: “Nataka nimwambie kwamba hakuna kilichokopwa kisha tukakosa kufanya jambo la maendeleo. Katika barabara na viwanja vya ndege vilivyosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, ndege zinaruka.”

Alisema kusingekuwa na viwanja vya ndege vilivyoboreshwa katika maeneo kama Tabora, Shinyanga na sehemu nyingine nyingi endapo mikopo hiyo isingetumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Jambo la kusema kwamba tunakopa lakini hatuna tunalolifanya ni jambo la uzushi lisilo na maana na la uchonganishi kati yetu sisi na Watanzania.

“Labda kiongozi huyu hapendi Watanzania niliowataja katika maeneo haya wapande ndege wakiwa kwenye viwanja vizuri vya ndege,” alisema Ulega.


Misitu, biashara ya kaboni

Hoja nyingine iliyotolewa na Chadema na kujibiwa na Serikali ni madai ya wananchi kuzuiwa kuingia katika misitu yao huku baadhi ya maeneo yakidaiwa kutengwa kwa ajili ya wawekezaji wa biashara ya kaboni.

Katika hoja hiyo, Chadema ilisema wananchi wanapaswa kuwa wanufaika wa kwanza wa rasilimali zilizopo katika maeneo yao na kwamba kuwazuia kuingia misituni ni kuwanyima haki yao ya kunufaika na rasilimali hizo.

Madai hayo yalijibiwa Juni 23 mwaka huu bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji.

“Rais Samia ameanzisha Kituo cha Kaboni pale Morogoro. Cha pili, aliruhusu kuandaliwa kwa sheria husika na hakuna misitu iliyohifadhiwa iliyoingizwa katika biashara ya kaboni.

“Kwa hiyo kama wanayo mifano ya maeneo hayo wayataje. Wasizue na kuleta taharuki kwa wananchi. Tunalinda hifadhi zetu na tunalinda masilahi ya wananchi,” alisema.

Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuwaandaa wataalamu ili kuhakikisha nchi inakuwa na uwezo wa kusimamia sekta hiyo na kwamba biashara ya kaboni inafanyika kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa ujumla, ziara za kisiasa zimeongeza ushindani wa kisiasa nchini huku ikionyesha namna mijadala ya sera, maendeleo na mageuzi ya kisiasa inavyoendelea kutawala anga la kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2030.