Man United yaingia hofu hatihati kumkosa Sesko
Muktasari:
- United ilimleta kwa dau la paundi milioni 74 kama mshambuliaji wa kutegemewa baada ya kumpeleka Rasmus Hojlund kwa mkopo Napoli.
Manchester, England. Manchester United ina hofu kuwa mshambuliaji wake Benjamin Sesko anaweza kuwa nje hadi mwezi mmoja baada ya kuondolewa uwanjani akiwa anachechemea katika sare ya 2-2 dhidi ya Tottenham Hotspur kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
United ilimaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya Sesko kuumizwa goti wakati Ruben Amorim akiwa ameshatumia nafasi zote za mabadiliko.
Ingawa vipimo vimeonyesha hakuna madhara makubwa, taarifa zinaeleza kuwa huenda Sesko akakaa nje kwa takribani wiki tatu hadi nne, na klabu bado haijaweka muda maalumu wa kurejea kwake. Staa huyo wa miaka 22 amejiondoa pia kwenye kikosi cha Slovenia ili aanze programu ya matibabu huko Carrington.
Kwa sasa United hawana uhakika wa kurejea kwake uwanjani, ikizingatiwa hili ndilo jeraha lake la kwanza kubwa tangu atue Old Trafford msimu huu. United inamatumaini kuwa atapona kabla ya wakati ambao Bryan Mbeumo, Amad Diallo na Noussair Mazraoui watakuwa wakielekea katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika 9AFCON), ili kuzuia pengo kubwa kwenye safu ya ushambuliaji.
Kocha Amorim hakuficha hofu yake mara baada ya mchezo dhidi ya Spurs:
“Nimekuwa na wasiwasi kwa sababu jeraha lipo kwenye eneo la goti. Tunamhitaji Benjamin ili timu yetu iendelee kuwa imara zaidi. Tunahitaji kufanya vipimo vyote ili kuelewa nini kimetokea,” alisema Amorim.
Kutokana na hali hiyo, Amorim atalazimika kuwa mbunifu katika eneo la ushambuliaji akiwa na wachezaji wachache wa asili ya kucheza kama namba tisa.
Matheus Cunha ndiye anayetarajiwa kuziba pengo kama mshambuliaji wa kati, kama alivyofanya dhidi ya Tottenham, huku Joshua Zirkzee ambaye amekuwa akilalamikia kukosa muda wa kutosha uwanjani akitarajiwa kupata nafasi zaidi.
Mason Mount pia atahitaji kuwa fiti ili kusaidia kuziba mapengo yatakayoachwa na Mbeumo, Amad na Sesko.
Sesko amekuwa akipokea ukosoaji mkubwa tangu atue England, wakiwemo wachambuzi kama Gary Neville. Hadi sasa amefunga mabao mawili na kutoa asisti moja kwenye mechi 11 za Premier League.
United ilimleta kwa dau la paundi milioni 74 kama mshambuliaji wa kutegemewa baada ya kumpeleka Rasmus Hojlund kwa mkopo Napoli.