Man United, Spurs, Chelsea zatinga kibabe fainali Ulaya

Muktasari:
- Fainali ya Europa League msimu huu itafanyika katika Uwanja wa San Mames jijini Bilbao, Hispania.
Timu tatu zinazoshiriki Ligi Kuu England (EPL) zimefanikiwa kutinga fainali ya mashindano ya Kombe la Europa League na Kombe la UEFA Conference baada ya jana Mei 8, 2025 kupata ushindi kwenye mechi za marudiano za mashindano hayo. Timu hizo ni Manchester United, Tottenham Hotspur na Chelsea.

Hata hivyo Manchester United ambayo imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumba Old Trafford dhidi ya Athletic Bilbao, imetinga fainali ya Kombe la Europa League kwa heshima kwa vile imelinda rekodi yake ya kuwa timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote katika mashindano ya Ulaya msimu huu.

Mabao ya Mason Mount aliyefunga mawili na mengine ya Rasmus Hojlund na Casemiro yameifanya Man United kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 ambao umechangia timu kufikisha mechi 14 bila kupoteza ambapo wamepata ushindi mara nane na kutoka sare sita.
Manchester United imefuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1 kwa vile mechi ya kwanza ugenini waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Katika fainali ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa San Mames, Hispania, Mei 21, mwaka huu, Man United itaumana na Tottenham Hotspur ambayo jana imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini huko Norway dhidi ya Bodo/Glimt.

Mabao ya Spurs kwenye mechi hiyo yamefungwa na Dominic Solanke na Pedro Porro.
Spurs imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1 kwani mechi ya kwanza walishinda mabao 3-1 nyumbani wiki iliyopita.
Katika kombe la UEFA Conference League, Chelsea ilipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Stamford Bridge dhidi ya Djugarden ya Sweden na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1.

Katika mchezo wa kwanza ugenini, Chelsea iliibuka na ushindi wa mabao 4-1. Bao pekee la Chelsea katika mechi ya jana limefungwa na Kiernan Dewsbury-Hall.
Kwenye mechi ya fainali ambayo itafanyika Mei 28, mwaka huu katika Uwanja wa Slaska Wroclaw, Poland, Chelsea itacheza dhidi ya Real Betis.
Betis imefuzu kwa kumtoa bingwa mtetezi Fiorentina kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 ambapo mechi ya kwanza iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na mechi ya marudiano zimetoka sare ya mabao 2-2.