Man City yatwaa ubingwa wa kihistoria

Hatimaye Manchester City imefanikiwa kutwaa ubingwa wa nne mfululizo wa Ligi Kuu England baada ya kuichapa West Ham mabao 3-1 kwenye mchezo wa mwisho wa ligi huku Arsenal ikiibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Everton nyumbani.
Man City imemaliza msimu ikiwa na pointi 91, Arsenal ikimaliza nafasi ya pili na pointi 89 ikiwa inashika nafasi ya pili nyuma ya City kwa mara ya pili mfululizo.
Man City ilifanikiwa kupata mabao mawili ya haraka kipindi cha kwanza kwenye Uwanja wa Etihad yaliyofungwa na Phil Foden huku West Ham ikirudisha moja mwishoni mwa kipindi hicho kupitia kwa Muhammad Kudus, lakini mwanzoni mwa kipindi cha pili ilifunga bao la tatu kupitia kwa Rodri na kumaliza kabisa matumaini ya Arsenal.
Arsenal ilianza kufungwa kwa bao safi la Idrissa Gana Gueye kipindi cha kwanza na kuwanyamazisha mashabiki waliokuwa wamejazana Emirates, lakini ikasawazisha dakika chache mbele kupitia kwa Takehiro Tomiyasu, hali ilizidi kuwaendea vizuri baada ya kufunga la ushindi kupitia kwa Kai Havertz hata hivyo bado bao hilo halikuwasaidia kutwaa ubingwa.
Sasa City chini ya Pep Guardiola, imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara nne mfululizo
Timu ambazo zimewahi kuchukua ubingwa mfululizo:
4 - Manchester City (2020/21 - 2023/24)
3 - Manchester United (2006/07 - 2008/09)
3 - Manchester United (1998/99 - 2000/01)
2 - Manchester City (2017/18 - 2018/19)
2 - Chelsea (2004/05 - 2005/06)
2 - Manchester United (1995/96 - 1996/97)
2 - Manchester United (1992/93 - 1993/94)
Matokeo mengine ya leo:
Brentford 2-4 Newcastle
Brighton 0-2 Manchester United
Burnley 1-2 Nottingham Forest
Chelsea 2-1 Bournemouth
Crystal Palace 5-0 Aston Villa
Liverpool 2-0 Wolves
Luton 2-4 Fulham
Sheffield United 0-3 Tottenham