Arsenal yafanya maandalizi ya kuvaa medali ubingwa EPL

Arsenal imeonyesha kuwa ina uhakika wa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England, Premier, baada ya jana jioni wachezaji na benchi la ufundi kufanya majaribio na kuvaa medali na kubeba kombe.
Arsenal yenye pointi 86, mbili nyuma ya Man City inatakiwa kuibuka na ushindi leo kwenye mchezo wake wa mwisho wa Ligi Kuu England dhidi ya Everton, lakini pia ikiwaombea Manchester City watoke sare au wapoteza dhidi ya wabishi West Ham kwenye Uwanja wa Etihad.
Jana baada ya mazoezi ya jioni, video zilionyesha jukwaa lililotengenezwa kwenye Uwanja wa Emirates na wachezaji wa timu hiyo wakawa wanapita na kuelekezwa jinsi ambavyo watasalimia na kuvaa medali, lakini ni nani atapokea kombe na wapi wataelekea kushangilia na mashabiki.
Kama Arsenal itafanikiwa kutwaa ubingwa huu, itakuwa ni mara yao ya kwanza tangu mwaka 2004 ilipobeba kombe ikiwa chini ya kocha Arsene Wenger, lakini ikiwa tofauti ina maana kuwa Man City itaweka rekodi ya kutwaa ubingwa huo kwa mara ya nne mfululizo.
Hata hivyo, ratiba inaonyesha kuwa kama timu hiyo itatwaa ubingwa basi maalumu la kushangilia litapita kwenye mitaa ya Islington London kesho asubuhi.