Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwisho wa ubishi EPL leo

Msimu wa 2023/2024 unafikia tamati leo kwa Ligi tatu tofauti barani Ulaya huku tukio la kumalizika kwa Ligi ya England (EPL)  msimu huu ndio likionekana kuteka hisia za kundi kubwa la wadau na mashabiki wa soka duniani kulinganisha na nyingine mbili ambazo nazo leo zitafikia tamati.

Ligi nyingine mbili ambazo nazo leo zinahitimisha msimu ni ile ya Ufaransa 'Ligue 1' na Ligi Kuu ya Uholanzi 'Eredivisie' ambazo mechi zao za kufunga msimu zitachezwa kuanzia muda mmoja kama ilivyo EPL ili kuepuka masuala ya upangaji wa matokeo.


EPL kiboko yao

Wakati Ligi nyingi zikiwa zimeshapata bingwa kabla hata ya msimu kumalizika kama ilivyo kwa ligi ya Ufaransa na Uholanzi ambazo leo zinakamilisha hesabu, shughuli inaonekana kuwa pevu kwa ligi ya England kwa vile hadi sasa haipata bingwa wake na dakika 90 za leo ndizo zitakazomaliza ubishi.

Idadi ya mechi 10 za ligi hiyo leo zitachezwa katika viwanja na miji tofauti nchini England ambapo zote zimepangwa kuchezwa kuanzia saa 12:00 jioni

Manchester City inayoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 88, inahitaji ushindi wa aina yoyote ile nyumbani dhidi ya West Ham United ili iweze kutwaa ubingwa kwani itafikisha pointi 91 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote msimu huu.

Lakini kama itateleza na kupoteza au kutoka sare, Manchester City inaweza kujikuta ikitema taji mbele ya Arsenal ambayo iko katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 86.

Kitendo cha kuwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, kinaipa matumaini Arsenal kwamba bado ina nafasi ya kutwaa ubingwa leo ikiwa itaibuka na ushindi katika mechi ya nyumbani dhidi ya Everton na Manchester City ikafanya vibaya dhidi ya West Ham.

Na kwa vile Arsenal na Man City kila moja ina uwezekano wa kutwaa ubingwa, bodi ya ligi ya England imeamua kwamba kwenye kila uwanja ambako timu hizo mbili zinacheza leo, kutakuwa na kombe moja bandia na medali 40 ambazo itapewa timu itakayofanikiwa kutwaa ubingwa.

Vita nyingine tamu leo ni ile ya kuwania nafasi ya tano kwa ajili ya ushiriki wa mashindano ya Ligi ya Europa ambayo inazihusisha Tottenham Hotspur iliyo nafasi ya tano na pointi zake 63 dhidi ya Chelsea iliyo nafasi ya sita na pointi 60.

Spurs inahitaji matokeo ya sare au ushindi katika mechi yake dhidi ya Sheffield United ambayo tayari imeshashuka daraja ili imalize katika naafsi hiyo lakini kama itapoteza inaweza kujikuta ikienguliwa na Chelsea ambayo yenyewe inacheza nyumbani dhidi ya Bournemouth.


Miujiza kuwabeba Luton, Palmer

Ni maajabu tu yanayoweza kuiokoa Luton leo na kusalia EPL msimu ujao vinginevyo itaungana na Burnley na Sheffield United ambazo tayari zimeshaaga ligi hiyo.

Luton inazidiwa kwa pointi tatu na Nottingham Forest iliyo katika nafasi ya 17 na ili ibakie, inapaswa kuombea wapinzani wao hao wapoteze dhidi ya Burnley kwa idadi kubwa ya mabao na wao waibuke na ushindi mnono mbele ya Fulham ili waweze kubakia.

Hadi sasa Nottingham Forest yenye pointi 29, utofauti wa mabao yake ya kufunga na kufungwa ni -19 wakati Luton iliyo na pointi 26, tofauti yake ya mabao ya kufunga na kufungwa ni -31.

Muujiza mwingine ambao unasubiriwa kwa hamu kuona kama unaweza kutokea au la ni ule wa nyota wa Chelsea, Cole Palmer kumpiku Erling Haaland wa Manchester City kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu ambacho hutolewa kwa mshindi wa tuzo ya mfungaji bora wa msimu.

Haaland ameshapachika mabao 27 na Palmer akimfuatia kwa kufunga mabao 22 na anayeshika nafasi ya tatu ni Alexander Isack wa Newcastle United ambaye amepachika mabao 20.

Ikumbukwe tuzo ya kipa bora wa msimu tayari imeshanyakuliwa na David Raya wa Arsenal kutokana na namba ya michezo ambayo hajaruhusu bao kutoweza kufikiwa na kipa mwingine yeyote.


Ufaransa

Msimu wa Ligi Kuu Ufaransa 2023/2024 nao unafungwa leo huku mechi hizo za mwisho zikionekana kutokuwa na presha kubwa kwa timu kutokana na mbio za kuwania nafasi na tuzo tofauti kuwa zimeshaamriwa kabla hata ya raundi ya mwisho.

Tayari PSG imeshatwaa ubingwa huku Monaco ikijihakikishia nafasi ya pili na timu ambayo ina uhakika wa kumaliza katika nafasi ya tatu ni Lille.

Kuna utofauti wa mabao nane kati ya kinara wa ufungaji Kylian Mbappe ambaye amefunga mabao 27 akifuatiwa na Jonathan David wa Lille aiyefunga mabao 19 jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa Mbappe ana zaidi ya asilimia 99 kumaliza akiwa mfungaji bora msimu huu.


Uholanzi hakujapoa


Ligi nyingine ambayo msimu huu unamalizika leo ni ile ya Uholanzi 'Eredivisie' ambapo idadi ya mechi tisa zitachezwa katika viwanja tofauti kuanzia saa 9:30 alasiri kila moja.

Mabingwa wa ligi hiyo msimu huu, PSV watakuwa nyumbani kuikaribisha RKC Waalwijk, Almere City itacheza na NEC, Volendam itakabiliana na Go Ahead Eagles, Feyenoord itakuwa mwenyeji wa Excelsior wakati huo Heracles ikikabiliana na Fortuna Sittard.

Mechi nyingine leo za kufungia msimu wa Eredivisie ni kati ya PEC Zwolle dhidi ya FC Twente, Sparta Rotterdam itacheza na Heerenveen na Vitesse itaikaribisha Ajax.

Kinachosubiriwa kwa hamu katika mechi za leo ni kupatikana kwa mchezaji atakayeshinda tuzo ya mfungaji bora msimu huu kutokana na ushindani mkali uliopo baina ya Vangelis Pavlidis na Luuk de Jong.

Kwa sasa Pavlidis anayeichezea AZ Alkamaar ndiye kinara wa kufumania nyavu akiwa amefunga mabao 28 na De Jong wa PSV, anamnyemelea kwa ukaribu akiwa ampechika mabao 27.

Tayari timu za Vitesse na Volendam zimeshashuka daraja huku PSV na Feyenoord zikiwa zimeshajihakikisha tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.


Ratiba leo

Ligi Kuu England-EPL

Arsenal vs Everton (Saa 12:00 jioni)

Brentford vs Newcastle United (Saa 12:00 jioni)

Brighton vs Man United (Saa 12:00 jioni)

Burnley vs Nottingham Forest (Saa 12:00 jioni)

Chelsea vs Bournemouth (Saa 12:00 jioni)

Crystal Palace vs Aston Villa (Saa 12:00 jioni)

Liverpool vs Wolves (Saa 12:00 jioni)

Luton vs Fulham (Saa 12:00 jioni)

Man City vs West Ham (Saa 12:00 jioni)

Sheffield United vs Tottenham (Saa 12:00 jioni)