Man City, Man United zabanwa Spurs, Chelsea hoi
Muktasari:
- Leo utapigwa mchezo mmoja pale kwenye Uwanja wa Emirates ambapo wenyeji Arsenal watakuwa na kibarua kigumu kuikabili Liverpool.
Katika mikiki mikiki ya Ligi Kuu England iliyopigwa jana kwenye viwanja tofauti, ilishuhudiwa vigogo wakubwa wakibanwa mbavu baada ya kulazimishwa matokeo ya sare na vipigo.
Manchester City ambao walionekana kuwa ni wapinzani wa karibu wa Arsenal katika mbio za Ubingwa msimu huu hawakuweza kutamba mbele ya Brighton baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Etihad, Erling Haaland alikuwa wa kwanza kuipa Man City bao la uongozi katika dakika ya 41 kabla ya firimbi ya mapumziko kulia.
Hata hivyo, kipindi cha pili Brighton ilirejea kivingine na kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Kaoru Mitoma dakika ya 60.
Hadi firimbi ya mwisho inapulizwa vijana wa Pep Guardiola waliondoka wakiwa wamegawana pointi na Brighton.
Katika mchezo mwingine ilishuhudiwa Tottenham ikikubali kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Bournemouth ambao walikuwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Vitallity.
Bao la ushindi lilifungwa dakika za majeruhi na Antoine Semenyo ambaye alipachika bao la tatu na kuihakikishia timu yake kuondoka na pointi tatu muhimu.
United ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Tarf Moor dhidi Burnley ilijikuta ikibanwa baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2.
Mabao ya United yalifungwa na mshambuliaji, Benjamin Sesko ambaye aliingia wavuni mara mbili wakati beki, Ayden Heaven akijifunga kwa upande wa United huku Jaidon Anthony akifunga bao la kusawazisha kwa upande wa Burnley.
Chelsea ilikubali kipigo cha mabao 2-1 ugenini kwenye Uwanja wa Craven Cottage dhidi ya Fulham. The Blues ilipata pigo dakika ya 22 ambapo beki wake Marc Cucurella alitolewa nje ya mchezo kwa kadi nyekundu baada ya kumvuta mkono mshambuliaji wa Fulham, Harry Wilson ambaye alikwa karibu na eneo la hatari.
Mabao ya Fulham yalifungwa na Raul Jimenez katika dakika ya 55 akimalizia kwa kichwa pasi ya Sander Berge wakati Wilson akipachika bao la ushindi dakika ya 81 huku bao pekee la Chelsea likiwekwa kambani na mshambuliaji, Liam Delap.
Michezo mingine ilishuhudiwa Everton ikitoka sare ya 1-1 na Wolves, Newcastle ikiichapa Leeds mabao 4-3 wakati Aston Villa ikitoka suruhu na Crystal Palace huku Brentford ikiilaza Sunderland mabao 3-0.
Leo utapigwa mchezo mmoja pale kwenye Uwanja wa Emirates ambapo wenyeji Arsenal watakuwa na kibarua kigumu kuikabili Liverpool.