Shearer aikosoa Chelsea, amuonya kocha mpya
Muktasari:
- Shearer amesema lengo la Chelsea kwa sasa ni kufuzu Ligi ya Mabingwa, si kushinda ligi, akitabiri kuwa Manchester City na Arsenal ndizo zitatawala mbio za ubingwa.
Mshambuliaji wa zamani wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Alan Shearer, ameikosoa vikali klabu ya Chelsea, kufuatia kuondoka ghafla kwa kocha Enzo Maresca siku ya Mwaka Mpya.
Shearer pia ametoa onyo zito kwa kocha anayeongoza kwenye mbio za kurithi mikoba ya Maresca, Liam Rosenior, akisema atalazimika kufanya zaidi ya mafanikio ya mtangulizi wake ili kudumu Stamford Bridge.
Rosenior (41), ambaye kwa sasa ni kocha wa Strasbourg ya Ufaransa klabu inayomilikiwa na wamiliki wale wale wa Chelsea, BlueCo anatajwa kuwa chaguo namba moja kuchukua nafasi hiyo.
Shearer amesema kuondoka kwa Maresca kulimshangaza, lakini akabainisha kuwa kauli ya kocha huyo aliyodai kupitia kipindi kibaya zaidi cha saa 48 mwezi Desemba huenda ilichochea tetesi za mustakabali wake.
Shearer amesema kocha yeyote anayekubali kazi Chelsea lazima atambue kuwa ni klabu tofauti na nyingine kutokana na mfumo wa uendeshaji.
“Unapoingia Chelsea unajua kabisa unachokifanya. Sio klabu ya kawaida. Wamiliki wana mfumo wao kununua wachezaji vijana, kuwaendeleza, kuwapa mikataba mirefu isiyo ya kawaida na baadaye kuwauza,” amesema Shearer.
Shearer aliongeza kuwa mfumo huo hauwezi kuleta ubingwa wa ligi kirahisi, akisisitiza kuwa kocha mpya atalazimika kuzidi mafanikio ya Maresca, jambo analoona kuwa gumu.
Maresca, katika msimu wake, aliiongoza Chelsea kutwaa Kombe la Dunia la Klabu (FIFA Club World Cup) na Kombe la Conference League, pamoja na kuirudisha klabu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Alishinda mataji mawili, timu ilikuwa nafasi ya tano. Nafikiri alifanya kazi nzuri sana. Sina uhakika angefanya zaidi ya hapo,” amesema Shearer.
Akizungumzia hali ya ndani ya klabu, Shearer amesema:
“Chelsea wakati mwingine ni klabu ya hovyo sana. Hivyo ndivyo wamiliki wanavyotaka kuiendesha. Hakuna kinachonishangaza tena katika soka hasa Chelsea.”
Kwa upande wa Rosenior, kocha huyo alipohojiwa kuhusu mustakabali wake katika mkutano na waandishi wa habari Ijumaa, amesema hawezi kutoa dhamana ya kubaki Strasbourg.
“Maishani hakuna dhamana. Hujui kesho itakuwaje. Nafanya kazi yangu tu. Napenda klabu hii, lakini siwezi kutoa uhakika wa chochote,” amesema Rosenior.
Shearer amekiri kuwa Rosenior anaheshimika kutokana na kazi yake Strasbourg na Hull City, lakini akaibua swali iwapo ana uwezo wa kubeba presha ya klabu kubwa kama Chelsea.
“Swali kubwa ni: je, yuko tayari kwa kazi kubwa kama Chelsea? Tumeona kilichomtokea Graham Potter,” amesema.
Shearer amehitimisha kwa kusema kuwa lengo la Chelsea kwa sasa ni kufuzu Ligi ya Mabingwa, si kushinda ligi, akitabiri kuwa Manchester City na Arsenal ndizo zitatawala mbio za ubingwa.