Man City, Inter Milan zaondolewa Kombe la Dunia la Klabu

Muktasari:
- Kocha Pep Guardiola alionekana kuchanganyikiwa, akishindwa kuamini kilichokuwa kinatokea, huku mashabiki wa City wakibaki kimya.
Orlando, Marekani. Mabingwa wa Ulaya, Manchester City wamejikuta wakipgwa vikumbo katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa Al Hilal ya Saudi Arabia, katika mchezo uliopigwa usiku wa kuamkia leo katika Dimba la Exploria.

Kilichoikuta Man City ndicho kilichoikuta Inter Milan baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Fluminense kwenye Uwanja wa Bank of America, North Carolina na kukatisha ndoto za vigogo hao wa Italia kufika robo fainali.
City waliingia kwenye mchezo huo wakipewa nafasi kubwa ya kusonga mbele hasa baada ya Fluminense kuwaondoa Inter Miami na hivyo kuweka mazingira mepesi ya kufuzu hadi nusu fainali, ambako walitarajiwa kukutana na Chelsea.

Lakini mambo yaliwaendea kombo. Licha ya kuanza vizuri na kufunga bao la mapema kupitia Bernardo Silva katika dakika ya tisa, walijikuta wakiruhusu mabao mawili kwa haraka kipindi cha pili, huku safu yao ya ulinzi ikionekana kuyumba mno.
Malcom na Marcos Leonardo waliipa Al Hilal mabao mawili ya haraka haraka, kabla ya Erling Haaland kuisawazishia City katika dakika ya 55. Hata hivyo, Kalidou Koulibaly aliwarudisha Al Hilal mbele kwa bao la kichwa katika muda wa nyongeza baada ya kona ya Ruben Neves.

City walionekana kurejea mchezoni baada ya Phil Foden kusawazisha bao la tatu, akimalizia krosi ya Rayan Cherki, lakini haikutosha. Dakika nane kabla ya mchezo kumalizika, Sergej Milinkovic-Savic alifunga kwa kichwa, mpira ukitoka kwa Ederson na kuokolewa na Leonardo aliyemalizia kwa urahisi.
Kocha Pep Guardiola alionekana kuchanganyikiwa, akishindwa kuamini kilichokuwa kinatokea, huku mashabiki wa City wakibaki kimya. Kwa upande mwingine, Al Hilal waliandika historia kubwa kwa kuwaondoa mabingwa wa Ulaya na kuweka rekodi mpya kwa soka la Saudi Arabia.

Katika mchezo huo, Haaland alifunga bao lake la 41 kwa msimu huu, lakini alikosa nafasi nyingine mbili za wazi. Pia, aliumia mguu katika sehemu ya paja na kutolewa dakika za mwisho, huku Rodri naye akiondolewa uwanjani kwa tahadhari.
Mchezo huo unaacha maswali mengi kwa Guardiola na kikosi chake. Safu ya ulinzi ilionekana dhaifu, huku mabeki Ruben Dias na Joao Cancelo wakifanya makosa. Hali hiyo imeongeza wasiwasi kwa mashabiki wa City, ambao sasa watarejea nyumbani mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Thiago Silva alia kwa furaha Fluminense ikiing’oa Inter Milan
Nahodha wa Fluminense, Thiago Silva alishindwa kuzuia hisia zake na kulia kwa furaha baada ya kikosi chake kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Inter Milan na kufuzu robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu.
Silva (40), ambaye alirejea Fluminense mwaka jana baada ya miaka 15 ya mafanikio barani Ulaya, alicheza dakika zote 90 katika ushindi huo mkubwa uliopatikana kwenye Uwanja wa Bank of America, North Carolina.

Fluminense walipata bao la kuongoza mapema dakika ya tatu kupitia mpira wa kichwa cha Germán Cano aliyeunganisha krosi iliyopigwa na John Kennedy.
Licha ya Inter kuongoza kwa kumiliki mpira na kupiga jumla ya mashuti 16, walilazimika kusubiri hadi dakika za nyongeza kuona mchezo unazikwa kabisa baada ya mchezaji wa akiba, Hercules kufunga bao la mbali lililosababisha mashabiki kulia kwa furaha jukwaani.

Thiago Silva alionekana akilia machozi ya furaha na baadaye kupigwa picha akimbusu mke wake, Isabele, uwanjani baada ya kipyenga cha mwisho.
Akizungumza na DAZN baada ya mechi, Silva amesema: “Ninajivunia sana wachezaji wenzangu. Ilikuwa mechi ngumu sana, dhidi ya timu iliyocheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi mmoja uliopita. Hali ya hewa ilikuwa ya joto mno, si rahisi kucheza kwenye mazingira kama haya. Lakini Fluminense ni timu kubwa.”

Kwa upande wa Inter, mshambuliaji Lautaro Martinez alikiri kuwa walizidiwa kipindi cha kwanza na kushindwa kuhimili joto la uwanjani.
"Hatukuwa vizuri kabisa kipindi cha kwanza, tukaruhusu bao la mapema na kupoteza mipira mingi. Fluminense walicheza kwa kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza. Tulijitahidi sana kipindi cha pili, lakini joto lilikuwa kali na tulikuwa na uchovu wa akili pia," amesema Martinez.
Fluminense waliingia hatua ya mtoano baada ya kumaliza kileleni kwenye Kundi F kwa alama tano, wakiwalazimisha sare Borussia Dortmund na Mamelodi Sundowns na kuwafunga Ulsan HD.

Kwa sasa watakutana na Al Hilal ya Saudi Arabia katika robo fainali ya michuano hiyo mikubwa iliyoshirikisha timu 32 duniani.
Fluminense ni moja kati ya timu nne kutoka Brazil zilizoshiriki michuano hiyo msimu huu, pamoja na Palmeiras, Flamengo na Botafogo. Wote walitinga hatua ya 16 bora, ingawa Botafogo waliaga baada ya kuchapwa na Palmeiras, huku Flamengo wakifungwa na Bayern Munich kwa mabao 4-2. Palmeiras sasa watakutana na Chelsea katika robo fainali siku ya Ijumaa.