Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kane aibeba Bayern ikipenya robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu

Muktasari:

  • Kane, ambaye yuko kwenye msimu wake wa pili na Bayern, sasa ana jumla ya mabao 41 msimu huu.

Miami, Marekani. Nahodha wa England, Harry Kane, ameendelea kuwa moto wa kuotea mbali baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa Bayern Munich wa mabao 4-2 dhidi ya Flamengo kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Dunia la Klabu.

Katika mchezo uliopigwa usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Hard Rock, Bayern walipata bao la kwanza mapema katika dakika ya sita baada ya Erick Pulgar kujifunga mwenyewe kabla ya Kane kuongeza la pili kwa shuti kali la mguu wa kushoto likigonga ndani ya mwamba kabla ya kujaa wavuni.

Baada ya Leon Goretzka kuongeza bao la tatu la Bayern, Kane alirejea tena kipindi cha pili kufunga la nne safari hii akifanya hivyo kwa mguu wa kulia akimalizia pasi ya kutoka kwa Joshua Kimmich.

Flamengo walijitutumua kupitia bao la Gerson na penalti ya Jorginho aliyewahi kuzichezea Arsenal na Chelsea, lakini hawakuweza kuzuia ubabe wa Bayern waliotawala mchezo kwa kiasi kikubwa licha ya hali ya hewa ya joto kali.

Kane, ambaye yuko kwenye msimu wake wa pili na Bayern, sasa ana jumla ya mabao 41 msimu huu, ikiwa ni baada ya kufunga 44 msimu uliopita. Alikaribia kufunga hat-trick yake ya tisa akiwa na miamba hiyo ya Ujerumani, lakini kocha wake alimtoa dakika za nyongeza.

Hata hivyo, alitunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mchezo, ikiwa ni heshima ya mchango wake mkubwa kwenye ushindi huo muhimu.

Bayern vs PSG vita ya vigogo

Ushindi huo unaipanga Bayern kuvaana na Paris Saint-Germain (PSG) kwenye hatua ya robo fainali, baada ya mabingwa hao wa Ulaya kuichakaza Inter Miami ya Lionel Messi kwa mabao 4-0. PSG walipata mabao kupitia Joao Neves, Achraf Hakimi, na Tomas Aviles aliyejifunga.

Katika kuelekea mchezo wa robo fainali dhidi ya PSG Harry Kane amesema:

"Tutakutana na timu kali, PSG wamekuwa bora msimu huu. Lakini tuliwashinda awali msimu huu, na tunaamini tunaweza kufanya hivyo tena tukicheza kwa kiwango chetu. Tunahitaji kupumzika vizuri na kujiandaa kwa pambano hilo kubwa."

Kuhusu bao lake la pili, Kane alimsifia Kimmich:

"Ilikuwa pasi nzuri sana, ya kisiri. Nilipokea kwa mguso mmoja na nikachagua kupiga upande wa mbele bahati nzuri mpango ulichukua sura," amesema Kane.