Messi atolewa Kombe la Dunia la Klabu na timu yake ya zamani

Muktasari:
- Messi alionekana kuchanganyikiwa, akiwa ameshika mpira mara 14 tu katika kipindi cha kwanza.
Atlanta, Marekani. Nahodha wa Inter Miami, Lionel Messi, ameonja machungu ya kutolewa kwenye Kombe la Dunia la Klabu baada ya klabu yake ya zamani, Paris Saint-Germain (PSG), kuifunga timu yake ya sasa kwa mabao 4-0 katika mechi ya robo fainali iliyopigwa Jumapili usiku kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz, Atlanta.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz mjini Atlanta, PSG walithibitisha ubabe wao kama mabingwa wa Ulaya kwa kuwabomoa wakali hao wa Marekani waliokuwa wamealikwa kushiriki mashindano hayo na FIFA.

PSG walianza kwa kasi, wakifunga bao la kwanza dakika ya sita kupitia Joao Neves, kabla ya kuongezea la pili dakika ya 39. Dakika chache baadaye, Tomas Aviles alijifunga mwenyewe kabla ya Achraf Hakimi kufunga la nne katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza.
Nahodha wa Inter Miami, Lionel Messi (38), aliyecheza kwa miaka miwili PSG (2021-2023), alionekana kuchanganyikiwa, akiwa ameshika mpira mara 14 tu katika kipindi cha kwanza.
Wenzake wa zamani Barcelona Luis Suárez (37), Sergio Busquets (36), na Jordi Alba (36) nao walikuwa kivuli cha wachezaji, wakionekana kushindwa kabisa kuhimili kasi ya vijana wa Paris.

Beckham atuliza maumivu ya mkono kwa maumivu ya uwanjani
Beckham, mmiliki mwenza wa Inter Miami, alikuwepo uwanjani licha ya kuwa ametoka kwenye upasuaji wa mkono. Akizungumza kabla ya mchezo, amesema:
“PSG ni klabu ya kipekee kwangu. Nilimaliza soka langu huko, na najivunia sana leo kuwa na timu yangu inacheza dhidi yao. Huu ni wakati wa kipekee sana kama mmiliki, rafiki na mshirika.”
Hata hivyo, hakutarajia PSG kama familia yake ya zamani ingemwadhibu kwa staili ya aina hiyo.

Safari ya PSG yaendelea
Kwa ushindi huo, PSG sasa watachuana na mshindi kati ya Bayern Munich na Flamengo kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa duniani kwa ngazi ya vilabu.

Inter Miami walifuzu katika hatua ya makundi kwa kutoa sare dhidi ya Al Ahly (0-0) na Palmeiras (2-2), pamoja na ushindi dhidi ya Porto (2-1). Hata hivyo, PSG wamewatoa kwenye reli mapema mno kabla hata ya wageni hao kutoka Marekani kupumua.