Al Ahly yatupwa nje, Messi kuvaana na PSG Kombe la Dunia la Klabu

Muktasari:
- FC Porto na Al Ahly zinalazimika kufungasha virago bila ushindi wowote.
East Rutherford, Marekani. Baada ya Wydad Casablanca kutolewa juzi, matumaini ya Afrika kwenye Kombe la Dunia la Klabu yamezidi kufifia baada ya Al Ahly ya Misri kutupwa nje mapema alfajiri ya leo kufuatia sare ya mabao 4-4 dhidi ya FC Porto ya Ureno.

Matokeo hayo yameifanya Al Ahly kumaliza katika nafasi ya nne kwenye Kundi A kwa pointi mbili pekee, ikishindwa kufuzu hatua ya mtoano. FC Porto imemaliza ya tatu ikiwa na pointi sawa lakini tofauti ya mabao ikiwabeba. Timu zilizofanikiwa kusonga mbele ni wenyeji Inter Miami na Palmeiras ya Brazil, ambazo zilitoshana nguvu kwa sare ya 2-2 na kufikisha pointi tano kila moja.

Katika pambano hilo la kusisimua lilochezwa kwenye uwanja wa MetLife, East Rutherford, ilishuhudiwa mshambuliaji wa Al Ahly, Wessam Abou Ali, akiandika rekodi kwa kufunga mabao matatu yaani hat-trick. Goli la nne kwa miamba hiyo ya Misri lilifungwa na Ben Romdhane.

Hata hivyo, juhudi hizo hazikutosha kuwaletea ushindi baada ya Porto kusawazisha mabao hayo. Rodrigo Mora, William Gomes, Samu Aghehowa na Pepe waliifungia Porto, huku Pepe akifunga bao la kusawazisha dakika ya 89 kwa shuti kali la mguu wa kulia lililotinga wavuni kutoka nje ya eneo la hatari.

Abou Ali aliianza alfajiri yake kwa kufunga bao la kwanza kwa shuti la kona kutoka upande wa kushoto, kabla ya kuongeza la pili kwa penalti na kutupia tena dakika ya 53 kwa kichwa safi akiunganisha krosi ya Mohamed Hany. Lakini Gomes na Aghehowa waliisawazishia Porto mara mbili kabla ya Ben Romdhane kurudisha uongozi kwa Al Ahly dakika ya 64, bao lililotokana na pasi ya Achraf Bencharki.

Pepe alihitimisha kalamu ya mabao kwa Porto baada ya kupokea pasi ya Gabri Veiga na kumtungua kipa Mohamed El Shenawy, na kuipeleka Al Ahly nje ya mashindano kwa mshtuko mkubwa.

Kwa matokeo hayo, FC Porto na Al Ahly zinalazimika kufungasha virago bila ushindi wowote, zikiwa zimeambulia sare mbili na kupoteza mechi moja kila moja.

Messi kuivaa PSG hatua ya 16 bora.
Ilionekana kama Inter Miami ingeibuka kinara wa Kundi A baada ya kuongoza 2-0 dhidi ya Palmeiras ya Brazil, lakini mporomoko wa dakika za mwisho uliwatupa hadi nafasi ya pili na sasa Lionel Messi anakabiliwa na mtihani mgumu dhidi ya klabu yake ya zamani Paris Saint-Germain katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia la Klabu.

Luis Suarez alifungua karamu ya mabao kwa goli la kuvutia akimtoka beki wa Palmeiras kwa nguvu na ustadi kabla ya kutikisa nyavu kwa shuti la mguu wa kushoto. Mapema, alipenya kwa pasi iliyomuwezesha Tadeo Allende kufunga bao la kwanza ndani ya dakika 16.

Lakini ndoto ya kuongoza kundi hilo ilififia dakika ya 88 baada ya Maximiliano Falcon wa Miami alifanya makossa kwa kuupiga mpira vibaya kwa kichwa ambao ulimkuta Mauricio wa Palmeiras, aliyefyatua kombora lililomshinda kipa, Oscar Ustari na kusawazisha matokeo kuwa 2-2.

Awali, Palmeiras walikuwa wamerudisha matumaini dakika ya 80 kupitia kwa mshambuliaji Paulinho aliyeunganisha pasi safi ya Allan na kufunga bao la kwanza. Sare hiyo iliwafanya Miami kufikisha pointi tano, sawa na Palmeiras, lakini kwa tofauti ya mabao waliangukia nafasi ya pili.

Atletico Madrid yatupwa nje
Atletico Madrid imekuwa timu ya kwanza kubwa kutolewa katika Kombe la Dunia la Klabu, licha ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Botafogo ya Brazil katika mchezo wa mwisho wa Kundi B uliochezwa kwenye Uwanja wa Rose Bowl.

Licha ya ushindi huo, kikosi cha Diego Simeone kilihitaji kushinda kwa tofauti ya mabao matatu ili kufufua matumaini ya kufuzu hatua ya 16 bora, baada ya kipigo kizito cha mabao 4-0 kutoka kwa Paris Saint-Germain kwenye mchezo wa ufunguzi.

Kwa muda mrefu mechi hiyo ilionekana kumalizika bila mabao, hali iliyowafanya Atletico kuishiwa matumaini, hadi dakika ya 87 ambapo Antoine Griezmann, aliyeingia kipindi cha pili, alipachika bao. Hata hivyo, Botafogo walidhibiti dakika za mwisho kwa uhodari na kujihakikishia tiketi ya kuendelea mbele.

Kundi B sasa linaongozwa na PSG, waliowashinda Seattle Sounders ya Marekani kwa mabao 2-0 na kufuzu hatua ya mtoano wakiwa kileleni, wakifuatiwa na Botafogo.