Luis Miquissone naye afuata mamilioni Libya
Nyota wa kimataifa wa Msumbiji Luís Miquissone. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Al Ahly Benghazi inakuwa timu ya nane kwa Luis Miquissone kuichezea katika soka la ushindani ambapo nyingine sita alizowahi kuzitumikia hapo nyuma ni UD Songo, Mamelodi Sundowns, Al Ahly, Abha, Royal Eagles, Chippa United na Simba.
Dar es Salaam. Nyota wa kimataifa wa Msumbiji Luís Miquissone, leo, Ijumaa Januari 23, 2026, atasaini mkataba na Al Ahly Benghazi ambayo ni miongoni mwa klabu kongwe nchini Livya ikishiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Uhamisho huo unakuja baada ya kiwango bora ambacho winga huyo amekionyesha akiwa na UD Songo, ambayo aliiongoza kutwaa taji la Ligi Kuu ya Msumbiji msimu uliopita, Kombe la Msumbiji, pamoja na tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Msumbiji.
Mkataba baina ya Miquissone na Al Ahly Benghazi utasainiwa baada ya kufanyika na kukamilika kwa vipimo vya kawaida vya afya. kwa mchezaji huyo.
Changamoto hii mpya katika klabu ya Al Ahly Benghazi, mojawapo ya klabu zenye heshima kubwa katika soka la Libya, inaashiria hatua nyingine muhimu katika safari ya kimataifa ya mshambuliaji huyo, ambaye amewahi kucheza katika klabu kama Al Ahly ya Misri na Simba SC ya Tanzania.
Takwimu za Miquissone msimu uliopita zinaonesha wazi mchango wake mkubwa, baada ya kufunga mabao 17 katika michezo 27 ya mashindano rasmi akiwa na kikosi cha UD Songo..
Ufanisi huo ulikuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya mataji mawili ya UD Songo na ulimthibitisha mchezaji huyo kama mhimili mkuu wa safu ya ushambuliaji.
Na tayari UD Songo imeshampata mrithi wa Miquissone ambaye ni mshambuliaji Brito Luís Arrumação kutoka Nacala Railway.
Hii ni mara ya tatu kwa Luis Miquissone kuachana na UD Songo na kutafuta malisho ya kijani nje ya nchi ya Msumbiji.
Mara ya kwanza ilikuwa ni 2018 alipojiunga na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na mara ya pili ilikuwa ni 2020 alipojiunga na Simba.
Al Ahly Benghazi inakuwa timu ya nane kwa Luis Miquissone kuichezea katika soka la ushindani ambapo nyingine sita alizowahi kuzitumikia hapo nyuma ni UD Songo, Mamelodi Sundowns, Al Ahly, Abha, Royal Eagles, Chippa United na Simba.
Katika kikosi cha Al Ahly Benghazi, Miquissone anaenda kukutana na nyota wa zamani wa Azam FC, Gibril Sillah