Liverpool bingwa EPL 2024/25, yaibonda Tottenham Hotspur

Muktasari:
- Mara ya mwisho Liverpool kutwaa taji hilo ilikuwa msimu wa mwaka 2019/2020, na kusherehekea bila mashambiki wao uwanjani kutokana na uwepo wa mlipuko wa Uviko-19. Msimu huu wanatwaa kombe hilo mbele ya mashambiki zaidi ya 61,276 waliofurika katika uwanja wa Anfield.
Imeisha hiyo. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Liverpool kuibamiza Tottenham Hotspur mabao 5-1 katika mchezo uliopigwa dimba la Anfield.
Liverpool ambao sasa wanakuwa mabingwa wa EPL wakifikisha makombe 20 sawa na Manchester United, wametangaza ubingwa huo leo Jumapili Aprili 27, 2025.

Tottenham Hotspur ilianza kutangulia kupitia bao la kona lililofungwa na Dominic Solanke (12’), kisha Luiz Diaz kuweka sawa mzani kwa kumalizia pasi safi ya Dominic Szoboszlai (16’) na baadaye, Alexis MacAllister (24’) kunyoosha shuti kali lililomuacha Guglielmo Vicario mdomo wazi alipogeuka na kukuta nyavu zikitikisika.
Furaha ya mashabiki wa Liverpool walioujaza uwanja wa Anfield yalipomwagwa majivu ya ‘Legendari’ wao Billy Shanky iliongezeka baada ya Mholanzi, Cody Gakpo (34’) kupigilia msumari kisha kuvua fulana yake iliyoandika ‘Welcome to Jesus’ (karibu kwa Yesu). Gakpo amepigwa kadi ya njano kutoka na tukio hilo.
Mohammed Salah hakubaki mbali na goli la Tottenham Hotspur baada ya kuifungia Liverpool bao la nne (62’) na kukikaribia kiatu cha mfungaji bora wa EPL msimu huu kwa kufikisha mabao 28 kisha kuibua shangwe kwa mashabiki kisha kupiga nao ‘Selfie’.
Dakika ya 68’, mchezaji wa Spurs, Destiny Udogie amekoleza furaha kwa mashabiki wa Liverpool baada ya kujifunga.

Dakika 90 zimemalizika Liverpool 5-1 Tottenham Hotspur. Ni shangwe na bata tu nje ya Anfield muda huu.