Leicester kumrudisha Van Nistelrooy EPL

Muktasari:
- Van Nestelrooy aliiongoza Man United kupata ushindi kwenye mechi tatu kati ya mechi nne huku akitoa sare mechi moja ambapo mechi ya mwisho aliifunga Leicester mabao 3-0 kwenye Ligi Kuu.
Leicester, England: Klabu ya Leicester City inayoshiriki Ligi Kuu ya England huenda ikamtangaza aliyekuwa kocha msaidizi wa zamani wa Manchester United Ruud van Nistelrooy kuja kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo.
Van Nistelrooy anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Steve Cooper ambaye ametimuliwa klabuni hapo baada ya kudumu kwa siku 157 akiiongoza Leicester kucheza mechi 12 za Ligi Kuu ambapo ameshinda mechi mbili, ametoa sare mechi nne, akipoteza mechi sita, akivuna pointi 10 huku Leicester ikishika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi.
Kutimuliwa kwa Erik Ten Hag kwenye viunga vya United kulimfanya Van Nestelrooy kuwa kocha wa muda kabla ya ujio wa Ruben Amorim ambaye hakutaka kufanya kazi na mshambuliaji huyo wa zamani.
Van Nestelrooy aliiongoza Man United kupata ushindi kwenye mechi tatu kati ya mechi nne huku akitoa sare mechi moja ambapo mechi ya mwisho aliifunga Leicester mabao 3-0 kwenye Ligi Kuu.
Staa huyo aliwahi kuwa kocha mkuu wa PSV ya Uhoranzi ambapo aliiongoza kutwaa Kombe la Ligi msimu wa 2022-2023 kabla ya kujiunga na Man United akiwa msaidizi wa Erik Ten Hag.

Ben Dowson ambaye alikuwa msaidizi wa Steve Cooper anatajwa kuiongoza Leicester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Brentford utakaopigwa Jumamosi kabla ya ujio wa Van Nestelrooy.