Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man City yampasua kichwa Guardiola

Manchester, England. Pep Guardiola anaumiza kichwa zaidi kupata majibu ya nini kinaisibu Manchester City huku wachambuzi wa masuala ya soka wakibainisha kwamba kwa sasa timu hiyo imekuwa dhaifu na nyepesi kuruhusu mabao.

Hayo yanajiri baada ya Novemba 26, 2024 kushuhudia Man City ikiwa mbele kwa mabao 3-0 hadi dakika ya 70, lakini mchezo ukamalizika kwa sare ya 3-3 dhidi ya Feyenoord, wakiwa nyumbani Etihad katika usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Sare hiyo inaifanya Man City kwenda kuivaa Liverpool ugenini Uwanja wa Anfield Jumapili hii katika mchezo wa Premier League ikiwa na morali ya chini baada ya kutokuwa na matokeo mazuri katika michezo sita iliyopita katika mashindano tofauti.

City sasa imeruhusu mabao mawili au zaidi katika mechi sita mfululizo kwenye mashindano yote, kwa mara ya kwanza tangu Mei 1963.

Wakati Erling Haaland alipofunga bao la tatu kwa City dakika ya 53 dhidi ya Feyenoord, wenyeji walionekana kuwa kwenye njia nzuri ya kurudi katika wimbi la ushindi baada ya kupoteza mechi tano mfululizo zilizopita.

Hata hivyo, washindi hao wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023, walishindwa kuelewa jinsi walivyopoteza pointi mbili kutokana na sare hiyo iliyofanya mashabiki kuwapigia kelele za kutowaheshimu baada ya mechi kumalizika.

"Wanaonekana dhaifu," alisema Alan Shearer, nahodha wa zamani wa England, aliyeshuhudia mchezo huo akiwa Uwanja wa Etihad.

City haijawahi kushinda bila kuruhusu bao tangu Oktoba 26 mwaka huu, walipoichapa Southampton bao 1-0. Kuanzia hapo, wameruhusu mabao 17 katika mechi sita.

"Sijui kama ni jambo la kiakili," alisema Guardiola, ambaye alikasirishwa sana na mchezo wa timu yake kiasi cha kujikwaruza uso wake mwenyewe.

"Mechi ilikuwa nzuri wakati matokeo yakiwa 3-0, tulikuwa tunacheza vizuri, lakini kisha tukaruhusu mabao mengi kwa sababu hatukuwa thabiti. Tuliruhusu bao la kwanza na kisha jingine, ndivyo ilivyokuwa vigumu."

City inahitaji kupambana zaidi kama inataka kuepuka kucheza mechi ya mchujo ili kuendelea hatua ya 16 bora ya michuano hiyo kwani hivi sasa ipo nafasi ya 17 kati ya timu 36.

Timu hiyo inatakiwa kumaliza miongoni mwa timu nane bora za juu kwenye msimamo wa michuano hiyo ili kupata nafasi ya moja kwa moja kucheza hatua ya 16 bora. Ikumbukwe kwamba, timu zitakazomaliza nafasi ya 9 hadi 24 zitalazimika kucheza mechi za mtoano ili kupata timu nane zitakazoungana na zile za juu kutinga 16 bora.

Kwa sasa City imebakiwa na mechi tatu dhidi ya Juventus (Desemba 11, 2024), Paris St-Germain (Januari 22, 2025) na Club Brugge (Januari 29, 2025).

"Kwa sasa sipo tayari kufikiria kuhusu hilo, lazima tushinde mechi tatu za mwisho ili kumaliza miongoni mwa timu nane bora," aliongeza Guardiola.

"Tunahitaji kupona na kujiandaa kwa mechi ijayo. Ikiwa hatutakuwa na uwezo wa kushinda mechi kama tulivyofanya leo (juzi), itakuwa vigumu."