Man United yatua kwa nyota wa Sporting

Muktasari:
- Timu zinazomfukuzia Viktor Gyokeres ni Arsenal, PSG na Bayern Munich huku Man United ikipewa nafasi nzuri ya kuinasa saini ya mchezaji huyu ambaye anaweza kushawishiwa na kocha wake wa zamani Ruben Amorim.
Baada ya kumnasa kocha Ruben Amorim, Manchester United ipo kwenye mazungumzo na Straika wa Sweden, Viktor Gyokers anayekipiga Sporting CP ya Ureno.
Hayo yamejiri baada ya viongozi baadhi wa Man United kuonekana kwenye mchezo wa timu ya Taifa ya Sweden dhidi ya Azerbaijan inaripotiwa walienda kumfuatilia mchezaji huyo.
United inapewa nafasi kubwa ya kumnasa mchezaji huyu ambaye amewahi kufanya kazi na kocha Ruben Amorim kabla ya kutua kwenye viunga vya klabu hiyo huku ikielezwa huenda kocha huyo akamshawishi Viktor Gyokeres kujiunga na Mashetani Wekundu hao msimu ujao.
Viktor Gyokeres anatajwa kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari kwa sasa ambapo ameshacheza mechi 18, akifunga mabao 23 katika mashindano yote akiwa na Sporting msimu huu.
Kwenye michuano ya Ligi ya MabingwaUlaya amecheza mechi nne ambapo amefunga mabao matano kati ya hayo, mabao matatu alifunga kwenye mchezo mmoja dhidi ya Manchester City waliyopata ushindi wa mabao 4-1.
Kwenye Ligi Kuu ya Ureno Viktor Gyokeres amecheza michezo 11, akipachika mabao 16 na ndiye kinara wa mabao kama ilivyo kwenye mashindano ya timu za mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League) ambapo amefunga mabao tisa katika michezo sita ya kundi la Sweden.
Gyokeres alijiunga na Sporting CP msimu wa 2023/2024 akitokea Coventry City inayoshiriki Ligi daraja la kwanza England (Championship).