Leeds United, Burnley wageni wapya Ligi Kuu England

Muktasari:
- Timu nne zinaongoza kupanda Ligi Kuu England mara nyingi kuanzia 1992 zikiwa zimefanya hivyo mara tano kila moja ambazo ni Norwich, Leicester City, Burnley na West Bromwich Albion
Burnley na Leeds United zimerejea katika Ligi Kuu England (EPL) baada ya kupata ushindi katika mechi zao za ligi ya Championship zilizochezwa katika viwanja tofauti England.
Matokeo hayo ya jana, yamezifanya timu hizo kufikisha pointi 94 kila moja na hivyo kujihakikishia tiketi ya kushiriki EPL msimu ujao kwa vile hata zikipoteza mechi zao mbili zilizobaki, haziwezi kufikiwa na timu zilizo chini yao.

Burnley imerejea katika Ligi Kuu England baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sheffield United na hiyo inamaanisha imedumu katika Championship kwa msimu mmoja tu kwani ilishuka daraja kutoka EPL msimu uliopita.
Wakati Burnley wakidumu katika ligi ya Championship kwa msimu mmoja, Leeds United yenyewe imecheza kwa misimu miwili kwani ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu England msimu wa 2022/2023.
Kwenye Uwanja wa Turf Moor, wageni Sheffield United waliingia na matumaini ya kupata ushindi ambao ungewafanya wapunguze pengo la pointi baina yao na wenyeji wao Burnley kubakia tatu mabao lakini mabao mawili ya Josh Brownhill yameihakikishia ushindi Burnley ambao umeipa tiketi ya EPL msimu ujao.

Bao la kufutia machozi la Sheffield United limepachikwa na Thomas Cannon.
Katika Uwanja wa Elland Road, wenyeji Leeds United wamejihakikishia kupanda daraja kwa kutoa kichapo kizito cha mabao 6-0 kwa Stoke City, wafungaji wakiwa ni Joel Piroe aliyepachika mabao manne huku mengine mawili yakifungwa na Junior Firpo na Degnand Gnonto.
Kwa kufanikiwa kurudi EPL, Burnley inafikia rekodi inayoshikiliwa na Norwich City, West Bromwich Albion na Leicester City ya kuwa timu zilizopanda EPL mara nyingi zaidi kuanzia mwaka 1992 ambapo kila moja imepanda Ligi Kuu England mara tano.
Na katika kuthibitisha kuwa haijapanda Ligi Kuu England kwa kubahatisha, Burnley imeweka rekodi ya kuwa timu iliyocheza idadi kubwa ya mechi mfululizo bila kuruhusu bao (clean sheets) katika historia ya ligi ya Championship ambapo imefanya hivyo mara 12 msimu huu.
Kiujumla timu hiyo imecheza bila kuruhusu bao katika mechi 25 kati ya 44 za Ligi ya Championship ambazo imeshacheza hadi sasa.
Kwa kushindwa kupanda moja kwa moja kupitia nafasi mbili za juu, Sheffield United sasa itajaribu kusaka tiketi ya kucheza EPL ambayo itapatikana kwa mechi za mchujo zitakazohusisha timu iliyopo nafasi ya tatu hadi ya sita kwenye msimamo wa Championship.