VIDEO: Heche adakwa na Polisi Kariakoo, apelekwa Central

Muktasari:
- Ni baada ya kupanda jukwaani kwa ajili ya hotuba ya kampeni ya ‘No reforms, no election’ (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi)
Dar es Salaam. Mkutano wa hama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umeshindwa kufanyika baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche kukamatwa na Jeshi la Polisi muda mchache baada ya kupanda jukwaani kuanza kuhutubia umma.
Mkutano huo ambao ni mwendelezo wa kutoa elimu kuhusu kampeni yao ya ‘No reforms, no election’ (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) uliopangwa kufanyika Mtaa wa Mkunguni na Nyamwezi mkabala na Soko Kuu la Kariakoo.
Heche amekamatwa leo Jumanne, Aprili 22, 2025 mtaani hapo, muda mfupi baada ya kupanda jukwaani kuanza hotuba yake ya kampeni ya ‘No reforms, no election’ (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi).

Kabla ya kukamatwa kwake kulizuka majibizano kati ya Heche na polisi mmoja ambaye hakuvaa sare za jeshi hilo, akitambulika kwa jina (Peter) aliyemtaka kiongozi huyo kutii sheria bila shuruti kwa kutoendelea na mkutano katika eneo hilo, huku akieleza kutoa taarifa mapema ya kutofanya mkutano eneo hilo.
Pamoja na majibizano hayo, Heche aliendelea kuongea na wananchi kwa kile alichokuwa akisema wasimtishe, huku makada wengine wa chama hicho wakimkingia kifua kwa kudai taarifa walishatoa ya kufanyika mkutano huo.

Kadri muda ulivyokuwa unaenda katika mtaa huo wa Mkunguni na Nyamwezi ulipoanza kufanyika mkutano huo, polisi walikuwa wanaongezeka na baada ya nusu saa kupita Heche alikubali kuondoka katika eneo hilo.
Hata hivyo, Polisi waendelea kufuatilia gari iliyombeba kiongozi huyo na baadhi ya makada wakitaka kumkamata, walitembea umbali kiasi wakiendelea na majibizano ndipo Heche alikubali kwenda Kituo cha Polisi Msimbazi kwa sharti atembee pamoja na wanachama wake.
Alishuka kwenye gari na kuanza kutembea pamoja na makada wa chama hicho walipofika Kituo cha Polisi Msimbazi, makada wa chama hicho walifukuzwa na kubaki Heche na makada wanne.

Katika kituo hicho, hakuingia hadi ndani ya kituo cha Polisi ilikuja gari nyeupe (Toyota Pick Up) kisha alishuka askari mmoja na kumuamuru apande katika gari hiyo, lakini aligoma kwa kile alichodai hawezi kupanda peke yake bila mtu wa kumsindikiza.
Baadaye Polisi walikubali kupanda na kada mwingine kisha gari iliondoka katika kituo hicho kwenda uelekeo wa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), ambapo wanachama wengine walikuwa wanakodi usafiri kwenda huko.