Marcia Lewis, mwanamke wa shoka nyuma ya mafanikio ya Lewis-Skelly

Muktasari:
- Myles Lewis-Skelly, kijana mwenye umri wa miaka 18, amekuwa na mafanikio makubwa tangu aanze kucheza katika kikosi cha kwanza cha Arsenal msimu wa 2024/25.
Septemba 22, 2024, itabaki kwenye historia ya soka, hasa la England, kama moja ya siku za kipekee na kukumbukwa sana.
Ni siku ambayo Manchester City waliwakaribisha Arsenał dimbani Etihad katika moja ya mechi zilizojaa drama kubwa na ya hali ya juu.
Kuelekea mchezo huu kulikuwa na malumbano mengi sana kati ya kocha wa Arsenal Mikel Arteta, na kocha wa Manchester City - Pep Guardiola.
Wawili hawa waliendelea kuheshimiana hadi ilipokuja mechi hii ambapo mambo yakawa mengi na wakakaribia kuvunjiana heshima.

Lakini kati ya yote, hakuna tukio kubwa kama la dakika ya 65 pale mwamuzi Michael Oliver alipomuonesha kadi ya njano kijana wa miaka 17 aliyekuwa benchi, Myles Lewis-Skelly.
Kijana huyo ambaye hadi muda huo alikuwa hajacheza hata mechi moja ya ligi kuu, akajiandikia rekodi ya ajabu ya kupata kadi kabla ya kucheza hata mechi moja.
Kwa mujibu wa Gary Neville, aliyekuwa uwanjani pale kama mtangazaji wa uwanjani wa moja ya vituo vya luninga vinavyorusha matangazo, ni kwamba dogo alioneshwa kadi hiyo kwa kosa la kwenda kumwambia kipa wake, David Raya, ajifanye kaumia ili kupoteza muda.
Hata hivyo, dakika ya 90+2 dogo akaingia kuchukua nafasi ya Jurriën Timber. Mpira ukaisha na vurugu kuibuka kufuatia kauli ya dharau ya Haalad kwa Arteta, “Be humble, uh”...yaani “kuwa mpole”.

Wachezaji wa Arsenal wakamzonga Haaland, na dogo Myles akaunga pia. Haaland alipomuona, akashangaa na kuuliza, “who the f*ck are you”...yaani “wewe naye ni mpuuzi gani”
Ilipokuja mechi ya marudiano, Februari 2, 2025 ambayo Arsenal ilishinda 5-1, dogo alifunga bao la tatu na kushangilia kwa mtindo wa kukaa kama Haaland, na kusema, “now you know me, Haaland’, yaani sasa umenijua Haaland.

Lakini ukiacha hayo madrama, kama kuna kipindi ambacho dogo amegonga vichwa vya habari kwa mpira halisi, basi ni kwenye mechi mbili za robo fainali ya ligi ya mabingwa dhidhi ya Real Madrid.
Dogo alikiwasha hasa, si nyumbani si ugenini, akicheza kwa kujiamini licha ya umri wake mdogo wa miaka 19.
Mambo mengi yakazungumzwa hadi kufikia kuichimbua familia yake na kugundua siri kuu nyuma ya mafanikio haya.

Nyuma ya dogo huyu kuna Marcia Lewis, mama yake mzazi.
Licha ya kuwa mama mzazi wa dogo, amefanya kazi kubwa kuhakikisha mwanaye anapitia malezi sahihi ya soka.
Mwanaye alipoanza kuonesha mapenzi ya mpira na uelekeo mzuri, mama akaamua kuwekeza kichwani kwake kuujua zaidi mpira.
Dogo alipokuwa na miaka nane, alihudhuria akademi ya Chelsea, Tottenham na ya Arsenal. Familia ikaamua mtoto wao aende Arsenal ikiamini ni sehemu sahihi.
Alipofikisha miaka 11, simu zikaanza kuita kwa mama kutoka kwa mawakala mbalimbali, wakitaka kumsaini dogo.
Mama aliwakatalia kwa sababu sheria hairuhusu hadi mtoto afikie umri wa miaka 16.
Akiwa na maka 12, kampuni kadhaa za vifaa vya michezo zikaanza kumgombania zimpe mkataba wa viatu.
Hilo likawezekana alipofikisha miaka 14, pale aliposaini na kampuni ya Adidas. Hapo hapo Arsenal wakampa fursa ya kusomeshwa na klabu (scholarship), kitu ambacho hutakiwa kutokea kwa mtoto aliyefikisha miaka 16.

Mama akawakatalia Arsenal akiwaambia wasubiri kwanza hadi afikishe miaka 16...hakuna cha kukimbilia.
Sasa kuanzia hapo mama akaamua kwenda shule yeye mwenyewe ili ajue kila kitu kuhusu mpira ili amsaidie mwanaye.
Akaenda chuo kikuu cha Leeds Beckett University kusomea shahada ya umahiri ya biashara ya mpira (Masters in Football Business) na halafu akafanya mitihani ya FIFA ili kupata leseni ya uwakala wa wachezaji, akafaulu...lakini hakuchukua leseni hiyo kwa ajili ya kumsimamia mchezaji yoyote bali kupata elimu ya mpira ili ameze kumlea mwanaye vizuri.
Mama anasema kumlea mchezaji kunataka mlezi anayekujua vizuri mpira ili aweze kutatua changamoto zitakazomkabili kwani kila anapokua na changamoto zinaongezeka.
Anasema lengo lilikuwa kutengeneza mfumo utakaomfanya mwanaye aweke akili zake zote kwenye mpira.
Changamoto alizopitia kwenye malezi ya mwanaye na usumbufu wa mawakala, anasema asingependa kuona wazazi wengine wanapitia.
Mwaka 2023 akaanzisha mtandao wa no1fan.club, unaoendeshwa kama jukwaa, ambao ni la kwanza Uingereza kuongozwa na wazazi wenyewe.
Lengo la mtandao huu ni kuwasaidia wazazi kupenya katika kutafuta nafasi kwenye tasnia ya mpira kwa ajili ya watoto wao.
Ama kwa hakika mama Marcia Lewis ameifanya kazi kubwa na anastahili kupata tuzo ya kipaji bora wa ligi.