Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha wa Ujerumani amkingia kifua Wirtz

Berlin, Ujerumani. Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann, amesema kuwa matatizo ya Florian Wirtz tangu ajiunge na Liverpool yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira ya klabu hiyo hasa wachezaji wenzake na hali ya kutokuwa thabiti kwa kikosi cha Arne Slot.

Wirtz alisajiliwa kwa kishindo kikubwa majira ya kiangazi, Liverpool ikilipa pauni milioni 116 (Sh400 bilioni) kumtoa Bayer Leverkusen. Lakini tangu aingie kwenye Ligi Kuu England, mambo hayajamwendea vizuri kwani hajafunga wala kutoa pasi ya bao katika mechi zake 11 za ligi hadi sasa.

Bei yake kubwa imekuwa mzigo mzito, na mashabiki pamoja na wachambuzi wamekuwa wakimchambua kila wiki. Mechi dhidi ya Manchester City, ambayo Liverpool ilipoteza 3-0, ilizidisha shinikizo hilo baada ya Wirtz kucheza chini ya kiwango na kulazimika kubeba lawama.

Lakini Nagelsmann, ambaye amekuwa akimwamini kijana huyo na kumpa nafasi katika timu ya taifa amewataka wakosoaji wawe wavumilivu huku akitupa dongo kwa kocha Arne Slot.

“Kwa kuwa mkweli, hali iliyopo Liverpool haimfanyi iwe rahisi kwake,” amesema Nagelsmann katika mkutano wake wa kwanza na waandishi kabla ya mechi za kufuzu Kombe la dunia dhidi ya Luxembourg na Slovakia.

“Klabu yenyewe haiko imara kama ilivyokuwa mwaka jana. Ni vigumu kwa mchezaji mpya kuingia na kung’aa mara moja. Ukiangalia mechi dhidi ya City, walikuwa timu duni kwa dakika 90, kwa hiyo ni ngumu kwa Florian kuonyesha ubora wake.”

Akaongeza kuwa Wirtz anahitaji muda zaidi wa kuzoea jambo la kawaida kwa wachezaji wanaohamia Premier League.

“Tunajua anachoweza kufanya. Ni kawaida kwa kijana wa miaka 22 kupitia kipindi kigumu. Hawezi kucheza kwa kiwango cha juu kwa miaka mitatu mfululizo bila kupumua.”

Nagelsmann pia aliwatupia lawama wachezaji wa Liverpool kwa kukosa kutumia nafasi zinazotengenezwa na Wirtz:

“Pengine Liverpool wangeweza kumsaidia zaidi kwa kufunga baadhi ya nafasi anazowaandalia. Kwa sababu anazibuni nafasi, ila kwa bahati mbaya, hawataki kupeleka mpira wavuni. Hilo nalo ni sehemu ya ukweli.”

Wliomkosoa Wirtz

Miongoni mwa waliomkosoa Wirtz vikali ni mchambuzi wa Sky Sports, Gary Neville, aliyesema:

“Tumekuwa tukimpa muda, tukisema bado kijana, bado anajifunza. Lakini huyu ni mchezaji wa pauni milioni 116! Ni lazima aonyeshe ubora. Amechezea timu kubwa, ni mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani lakini dhidi ya City, alionekana kama mtoto mdogo. Ni lazima apambane zaidi, aonyeshe ukomavu.”

Kauli hiyo inaendana na aliyoyasema kiungo wa zamani wa Uholanzi Wesley Sneijder, aliyemwonya kuwa “ataishia kupotea kabisa Liverpool ikiwa hatabadili kasi yake haraka.”

Baba yake amtetea

Lakini upande wa familia unamuuunga mkono Nagelsmann. Baba wa Wirtz, ambaye pia ni meneja wake, amesema:

“Tangu mwanzo tulijua mechi kumi za mwanzo zitakuwa za majaribio. Florian yuko sawa kabisa. Kasi, umbali wa kukimbia na mtindo wa mchezo England ni tofauti kabisa si kama Bundesliga. Anajifunza hatua kwa hatua.”