Roy Keane: Liverpool ipo kwenye mgogoro mkubwa
Muktasari:
- Liverpool tayari imepoteza mechi tano msimu huu na inashika nafasi ya nane ikiwa pointi nane nyuma ya vinara Arsenal
Aliyekuwa nahodha wa Manchester United, Roy Keane, ametoa kauli kali dhidi ya Liverpool baada ya kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Manchester City, akisema wazi kuwa Majogoo hao wa Anfield wako kwenye mgogoro.
Liverpool, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, tayari wamepoteza mechi tano msimu huu na wanashika nafasi ya nane wakiwa pointi nane nyuma ya vinara Arsenal hali ambayo Keane amesema ni ya kutia wasiwasi.
Akizungumza kupitia Sky Sports, Keane amesema:
“Kwa sasa huwezi kuwaweka Liverpool kwenye mazungumzo ya ubingwa. Hiyo ni mechi ya tano wamepoteza. Angalia aina ya mabao wanayofungwa watu wanazungumzia washambuliaji wao, lakini upande wa ulinzi umevurugika kabisa.
Kiasi cha mabao wanayoruhusu ni cha kutisha. Hii itakuwa moja ya vipigo vibaya zaidi kwao. Mechi nyingine walifungwa dakika za mwisho, lakini hii itawauma sana. Kwa kweli, huu ni wakati wa mgogoro kwa Liverpool.”
Wakati huo huo, beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, naye hakubaki kimya. Alimlenga moja kwa moja beki wa Kifaransa Ibrahima Konate, akisema ndiye chanzo cha matatizo mengi kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo.
“Sielewi kabisa Konate anajaribu kufanya nini,” amesema Carragher. “Kila mara Liverpool wakifungwa au wakipatwa na shida, yeye huwa katikati ya tatizo. Msimu huu amekuwa hafanyi vizuri hasa wanapokuwa ugenini.”
Keane aliendelea kuikosoa Liverpool akisema mafanikio yao ya hivi karibuni dhidi ya Aston Villa na Real Madrid hayana maana yoyote baada ya kipigo hicho kizito.
“Kupoteza mechi tano kati ya kumi kwa klabu kama Liverpool ni mgogoro mkubwa. Man City walionekana imara zaidi, wenye ubora wa kiufundi na nguvu. Liverpool walionekana dhaifu, maamuzi mabovu, kasi ndogo walikuwa timu iliyopoa.”
Kwa ushindi huo, Man City imepanda hadi nafasi ya pili wakiwa pointi nne tu nyuma ya Arsenal, na Keane ameipongeza timu hiyo akisema inaonekana kurejea kwenye ubora wake wa zamani.
“City walikuwa bora sana. Hii ilikuwa kama zile City za zamani imara, zenye uzoefu na njaa ya ushindi, Liverpool wameboreshwa mechi chache zilizopita, lakini ukienda Etihad, unakutana na timu ya kiwango kingine.
“Nafikiri Arsenal wataangalia mechi hii na kuona wazi kuwa Man City wamerudi kwenye ubora wao,” amesema Keane.