Kocha Al Ahly afukuzia rekodi Afrika

Muktasari:
- Marcel Koller anaweza kufikia rekodi iliyowekwa na kocha wa zamani wa timu hiyo Pitso Mosimane ambaye aliifikisha Al Ahly kwenye hatua ya fainali mara tatu mfululizo.
Zimebaki saa chache kabla ya mchezo wa pili wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Al Ahly na Mamelodi Sundowns baada ya timu hizo kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliochezwa Afrika Kusini wiki iliyopita.
Iwapo Al Alhy itafanikiwa kufuzu fainali katika mchezo kocha wao Marcel Koller atafikia rekodi iliyowekwa na kocha wa zamani wa timu hiyo, Pitso Mosimane ambaye aliifikisha hatua ya fainali mara tatu mfululizo.

Mosimane raia wa Afrika Kusini aliiongoza timu hiyo kufika fainali mwaka 2020, 2021 na 2022 huku akifanikiwa kushinda mataji mawili mwaka 2020 na 2021.
Marcel Koller ana nafasi ya kuweka rekodi mpya iwapo atafika fainali na kuchukua ubingwa ambapo atakuwa kocha wa kwanza kushinda mataji matatu mfululizo huku Al Ahly ikiandika rekodi ya kutwaa mataji matatu mtawalia ikiwa haijawahi kufanya hivyo tangu kuanzishwa kwake.

Kocha huyu raia wa Switzerland ana mtihani wa kuvunja mwiko wa kutopata matokeo ya ushindi dhidi ya Mamelodi Sundowns tangu ajiunge na miamba hiyo ya Afrika kwani katika michezo mitano aliyocheza dhidi ya Mamelodi amepoteza mechi mbili na kupata sare mechi tatu.
Marcel Koller alianza kazi ya ukocha huko Switzerland ambapo amewahi kuzifundisha Klabu kama FC Basel, Grasshopper, na FC Wil kabla ya kujiunga na Al Ahly Septemba 9, 2022.

Mchezo mwingine wa nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika utakuwa baina ya Pyramids ambao watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani kukabiliana na Orlando Pirates ya Afrika kusini baada ya mchezo wa kwanza kutoka suluhu.

Iwapo Pyramids na Al Ahly zitafanikiwa kutinga katika hatua ya fainali itakuwa ni mara ya pili kwa taifa la Misri kutoa timu mbili kucheza fainali kwani mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2020 ambapo Al Ahly ilikutana na Zamalek katika hatua hiyo.
Kwa upande wa Afrika Kusini itakuwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo iwapo Mamelodi Sundowns na Pyramids zitatinga kwenye hatua ya fainali.