Refa Stellenbosch, Simba abadilishwa ghafla

Muktasari:
- Simba inahitaji ushindi ay sare ya aina yoyote dhidi ya Stellenbosch, Jumapili, Aprili 27, 2025 ili itinge hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya mabadiliko ya ghafla ya refa wa mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Stellenbosch na Simba itakayochezwa Jumapili, Aprili 27, 2025.
Awali refa aliyepangwa kuchezesha mechi hiyo alikuwa ni Amin Omar kutoka Misri na sasa timu hizo zitachezeshwa na Mohamed Maarouf Eid Mansour ambaye naye anatoka Misri.
Haijafahamika bado sababu za CAF kuchukua uamuzi huo wa kumbadilisha Amin Omar ambaye hana historia nzuri na Simba katika mashindano ya kimataifa.
Amin Omar ndiye alichezesha mechi ambayo Simba ilifungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Horoya katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/2024.
Kumekuwa na usiri mkubwa katika ufanyaji wa mabadiliko hayo na utangazwaji wake na CAF kuelekea mchezo huo uliobeba hisia na mvuto mkubwa kwa nchi za Afrika Kusini, Tanzania na Afrika kiujumla.
Mwamuzi Mansour atasaidiwa na wenzake kutoka Misri ambao ni Mahmoud Abouelregal na Ahmed Ibrahim ambao ilikuwa tangu awali wawe wasaidizi lakini pia kuna mabadiliko kwa refa wa akiba ambapo sasa atakuwa Mahmoud Nagy naye kutoka Misri.
Mtathmini wa marefa ni Bechir Hassani kutona Tunisia na Kamishina wa mechi ni Kelesitse Gilika wa Botswana.
Hakuna mabadiliko upande wa marefa wanaosimamia teknolojia ya video ya usimamizi kwa marefa (VAR) ambapo kuna Mahmoud Ashour na Mahmoud Elbana wote kutoka Misri.
Simba imewahi kukutana na refa Mansour mara mbili ambapo ya kwanza alikuwa refa wa kati ilipotoka sare ya bao 1-1 nyumbani na Asec Mimosas kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/2024 na mechi ya pili alikuwa refa wa akiba ilipoibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya msimu huohuo