Rais Samia abeba gharama za Simba Afrika Kusini

Muktasari:
- Simba inahitaji matokeo ya ushindi au sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano dhidi ya Stellenbosch, Aprili 27, 2025 ili itinge fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameipa Simba sapoti ya usafiri wa kwenda Afrika Kusini na kugharamia malazi kwa timu hiyo katika kipindi chote itakapokuwa huko kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch, Aprili 27, 2025.
Mechi hiyo ni ya marudiano ya hatua ya nusu fainali baada ya kwanza iliyofanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kumalizika kwa ushindi wa Simba wa bao 1-0.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji amethibitisha Rais Samia kutoa sapoti hiyo huku akitoa shukrani za klabu hiyo.
“Kwa niaba ya Klabu ya Simba Sports Club, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuiwezesha klabu yetu kushiriki mashindano ya kimataifa.
“Tumepokea kwa moyo wa shukrani mchango wa malazi na usafiri kwa ajili ya mchezo wetu wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch.
“Klabu ya Simba inatambua na kuthamini kwa dhati juhudi za Rais Samia katika kumarisha sekta ya michezo hapa nchini, hususan mpira wa miguu,” amesema Dewji.
Dewji amesema kuwa sapoti ya Rais Samia na Serikali imekuwa chachu kubwa ya mafanikio kwao na soka la Tanzania.
“Tumetiwa moyo pia na motisha ya Goli la Mama, ambayo imekuwa chanzo cha hamasa na ari kwa wachezaji na mashabiki wetu,” ameongeza Dewji.