Prime
Gambo na Mchengerwa hapatoshi bungeni, Spika awapeleka kamati ya maadili

Muktasari:
- Mbunge huyo amesema pamoja na taarifa hiyo, lakini kuna maeneo ambayo anahisi hajatendewa haki akiomba kupewa nafasi ya kuweka mambo sawa lakini Spika akamtaka kuweka kila kitu kwenye Kamati.
Dodoma. Sakata la ubadhilifu wa fedha zilizoibuliwa na Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo bado ngoma nzito na sasa limepelekwa kwenye Kamati ya Maadili, Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameagiza kamati ianze kufuatilia kuanzia leo Jumatano, Aprili 23, 2025 hadi wiki ijayo taarifa itolewe ndani ya Bunge.
Maagizo ya Spika yametokana na kutokukubaliana kati ya Gambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ambaye ameliambia Bunge leo kuwa tuhuma zote zilizotolewa na mbunge huyo hazina mashiko.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akizungumza bungeni leo Jumanne Aprili 16,2025 jijini Dodoma.
Wawili hao walijikuta wakiingia katika mabishano hasa katika kipengere cha uvunjaji na ujenzi wa soko la Machinga kuhusu Sh800 milioni ambazo Gambo alisema zinakusanywa kwa mwezi wakati Mchengerwa amesema Sh850 milioni hukusanywa kwa mwaka katika soko hilo.
Waziri Mchengerwa jana Jumanne, Aprili 22, 2025 alipokuwa akihitimisha hoja yake, alidokeza ameunda timu ya kuchunguza na kwamba majibu aliyonayo yanaonyesha hakuna hata senti ya Serikali iliyoliwa.
Miradi ambayo iliibuliwa na Gambo kwamba kuna fedha zimetumika vibaya ni ujenzi wa jengo la utawala, ujenzi wa barabara ya kutoka Stand mpya kwenda Mbauda na ujenzi wa Soko la Machinga.
Gambo aliibua tuhuma hizo Aprili 16, 2025 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Gambo alisema Jiji la Arusha wanajenga jengo la utawala gharama zake za jumla hazipungui Sh9 bilioni ambalo baadhi ya viongozi wanalipigia debe.
“Jengo la ghorofa nane unajenga kwa Sh9 bilioni maana yake kila floo moja ni Sh1 bilioni na ushee kitu ambacho kama una akili nzuri hakiwezekani,” alisema.
Alisema ukiangalia wameingia mkataba juzi wa Sh6.2 bilioni ambapo katika ule mkataba kuna baadhi ya vipimo walivyoandika kwenye thamani ya makadirio ya ujenzi (BOQ) na kwenye utekelezaji ni tofauti.
Gambo aliomba kuongeza jicho za ziada kwenye usimamizi wa miradi kwa sababu Rais anatafuta fedha dunia nzima kwa ajili ya Watanzania, lakini badala ya kusimamiwa vizuri zinakwenda kuliwa na watu wachache, jambo ambalo halikubaliki.
Baada ya mchango huo, Spika Tulia alisema kutokana na uzito wa tuhuma hizo na Bunge haliwezi kuliacha kama mchango wa kawaida na kumwagiza Waziri Mchengerwa, kulifanyia kazi na taarifa yake kuiwasilisha bungeni.
Alichokisema Mchengerwa
Leo Jumatano, Aprili 23, 2025, mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, Waziri Mchengerwa amepewa fursa na Spika Tulia kuwasilisha taarifa mbele ya Bunge hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa akizungumza bungeni leo Jumanne Aprili 16,2025 jijini Dodoma.
Amesema katika maeneo yote manne ya tuhuma dhidi ya ubadhirifu wa fedha za miradi ambazo ziliibuliwa na Gambo, zimekosa mashiko kwani hakuna senti hata moja ya Serikali ambayo ilitumika vibaya au kuliwa.
“Jengo la utawala lilianza katika kipindi ambacho Mheshimiwa Gambo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha mwaka 2019, lakini ujenzi ulianza mwaka 2021 baada ya kutoka kwenye mfumo wa force akaunti kwenda kwa mzabuni,” amesema Mchengerwa.
“Baadaye ujenzi huo ulihama kutoka force akaunti na kuingia mkandarasi mshauri ambaye akasaidia kupatikana kwa mkandarasi wa ujenzi na Gambo akiwa mbunge na hii ilitokana na malumbano yaliyokuwepo na kusababisha mradi kusimama,” amesema.
Hata hivyo, amemtuhumu mbunge huyo kuwa siku ya kikao cha kamati ya fedha wakati wakijadili kuanza kujenga kwa kutumia mzabuni, Gambo hakushiriki kwa ruhusa lakini taarifa zinaonyesha alilipwa posho ya kikao.
Mchengerwa amesema baadaye jengo hilo lilianza kujengwa baada ya mwaka 2023, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuingilia kati baadhi ya wahusika kuchukuliwa hatua na sasa jengo hilo liko ghorofa ya sita na fedha zilizolipwa ni kidogo ukilinganisha na uhalisia.
“Hakuna fedha ya Serikali iliyoibiwa mpaka sasa,” amesema Waziri Mchengerwa huku Gambo aliyekuwa bungeni akimfuatilia kwa umakini.
“Lakini kitu kingine, ni mbunge kutoa hoja ambazo zilishaibuliwa na baraza la madiwani ni sawa na kusema Serikali ni kipofu kwamba haioni lakini kumbe tunaona na tumefanyia kazi,” amesema Mchengerwa.
Kuhusu ujenzi wa soko, Waziri Mchengerwa amesema kila kitu kipo vizuri na tayari wamekamilisha mipango ya kutangaza zabuni Aprili 28, 2025 lakini wanaendelea na suala la maandalizi ya ujenzi wa soko la machinga kitalu B eneo la Bondeni jijini Arusha.
Baada ya taarifa hiyo, Spika ameomba ufafanuzi kuhusu kiasi cha Sh800 milioni kama ni mapato ya mwezi au mwaka ambapo Gambo aliweka msimamo wake ni mwezi wakati Mchengerwa akisema ni mapato ya mwaka.
Uamuzi wa Spika baada ya kuwapa wabunge wapige hesabu kwenye makusanyo ulithibitisha ni mapato ya mwaka jambo ambalo Gambo aliposimama alisisitiza tena ni Sh800 kwa mwezi.
Hii ni baada ya wabunge kupiga hesabu za Sh200,000 kwa vitanda vilivyopo kati ya 350 hadi 400. Hata hivyo, Waziri Mchengerwa akasema kwa mwezi ni Sh74 milioni kwa mujibu wa taarifa ya mkurugenzi wa halmashauri.
“Mheshimiwa Gambo katika mchango wake alisimama na kueleza kwa machungu na hapa ninamnukuu ‘eti mnakwenda kubomoa eneo ambalo linaingiza mapato ya Sh800 kwa mwezi’ yaani ni sawa na mbunge kujitoa katika sehemu hii,” amesema Dk Tulia.

Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo akizungumza bungeni leo Jumanne Aprili 16,2025 jijini Dodoma.
Spika amesema Bunge haliwezi kuvumilia taarifa ambazo linaona haziko sawa na kwamba kama mbunge atakuwa na hoja nyingine aendelee kuitoa kwa utaratibu unaotakiwa.
Spika Vs Gambo
Baada ya Spika kumaliza kutoa maelezo hayo, Gambo alisimama akiomba mwongozo wa Spika akisema, Waziri ametoa majibu na mimi nilitoa maelezo nikiomba uchunguzi ufanyike kutokana na tuhuma zilizokuwepo, sasa nilikuwa nadhani kuna mambo yamesemwa na nadhani hayakusemwa sawasawa.”
“Mosi kuhusiana na jengo la utawala, mheshimiwa Spika nilijenga hoja mbili,” amesema Gambo na kukatishwa na Spika akimweleza Gambo kuwa Waziri amesema taarifa isiyo sahihi.
Kisha Gambo akamwomba Spika amwache azungumze kama ambavyo Waziri Mchengerwa ameachwa. Hata hivyo, Spika akasema waziri ameachwa kwa sababu Gambo alichangia kwa kirefu bungeni na ulikuwa wasaa wa Serikali kusikilizwa na Bunge.
Kiongozi huyo wa Bunge akasema ikitokea Gambo akamruhusu basi itabidi na Waziri apewe fursa hiyo jambo ambalo amesema si utaratibu wa uendeshaji wa shughuli za Bunge.
Gambo akasimama akasema: “Kwanza amesema jengo lilianza nikiwa mkuu wa mkoa amesema uongo, lilianza nikiwa mbunge.”
Spika Tulia amesema maelezo yanaonesha lilianza mwaka 2019 ukiwa mkuu wa mkoa ni kweli? Gambo akasimama na kujibu si kweli ulianza mwaka 2021. Alipotaka kuendelea kuzungumza, Spika alimweleza akae.
Gambo akasema kuna maeneo anahitaji kutoa ufafanuzi zaidi ili kuweka sawa. Hata hivyo, Spika Tulia akasema, mbunge alipata fursa ya kusikilizwa, Serikali imetoa taarifa bungeni, lakini Gambo anasema amedanganya.
“Hili jambo sasa sina uwezo hapa wa kuanza kufuatilia kila mmoja, alipeleka kwenye kamati ya maadili kule atakwenda kusikilizwa. Kamati yetu itaanza kazi mara moja leo na wiki ijayo watapewa nafasi ya kuleta mrejesho hapa Bungeni.
Kamati itawasiliza na itasema nani mwongo na hatua za kuchukua itatuelekeza,” amesema Spika Tulia.
Baada ya maelezo hayo, Gambo akasimama tena kuomba mwongozo akisema: “Mimi naona kama sijatendewa haki kwa sababu…” kabla hajamaliza kuzungumza Spika akamweleza akae chini na suala hilo linakwenda kushughulikiwa kwenye kamati na wote yeye (Gambo) na Mchengerwa watasikilizwa huko.