KMC na Simba kupigwa Dar, busara yahusika

Muktasari:
- Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 63 wakati huo KMC ikishika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 30.
Dar es Salaam. KMC imeamua kuurudisha mchezo wake dhidi ya Simba, Mei 11, 2025 katika Uwanja wa KMC Complex badala ya kucheza Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Uamuzi huo umekuja baada ya timu hizo mbili kufanya mazungumzo ambayo yamefikia muafaka juu ya kubadilishwa kwa uwanja wa mechi.
Baada ya KMC kuamua kupeleka mechi hiyo katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Simba iliwapelekea ombi la mchezo huo kufanyika Dar es Salaam ili usiathiri safari yao ya kwenda Morocco kucheza mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane, Mei 17, 2025.
Baada ya majadiliano ya timu hizo mbili, makubaliano yamefikiwa kwa mechi hiyo kuchezwa katika Uwanja wa KMC Complex ili kuiwezesha Simba kusafiri mapema kwenda Morocco tofauti na iwapo ingechezwa Tabora.
Awali KMC kupitia Ofisa habari wake, Khalid Chukuchuku ilisema kuwa sababu mbili ndizo zimewafanya waamue kupeleka mechi hiyo katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
"Siku mbili baada ya kucheza na Simba, tutakuwa na mechi ya ugenini dhidi ya Tabora United katika Uwanja huohuo wa Ali Hassan Mwinyi hivyo benchi la ufundi limeshauri tukacheze hiyo mechi ili wachezaji wasichoshwe na safari.
"Lakini sababu ya pili ni kwamba kanuni zinaturuhusu kufanya hivyo na hii sio mara ya kwanza kitu kama hicho kufanyika," amesema Chukuchuku.
Kanuni ya 9(7) ya Ligi Kuu 2024/2025, kila timu inaruhusiwa kucheza mechi zake mbili za nyumbani katika uwanja uliopo katika mkoa tofauti na kituo ilipo.
"Timu ya Ligi Kuu inaweza kuteua viwanja vingine miongoni mwa viwanja vilivyokaguliwa na kukidhi vigezo vya kikanuni kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu kwa michezo yake miwili tu ya nyumbani na kuwasilisha Uteuzi wake huo siku ishirini na moja (21) kabla ya mchezo husika inayokusudia kucheza kwenye uwanja wa uteuzi.