Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba inavyopita njia ya miiba kuisaka nchi ya ahadi

Muktasari:

  • Mara ya mwisho kwa Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa ni msimu wa 2020/2021 ambapo pia ilitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania.

Wana wa Israel walitumia takribani miaka 40 kwa safari ya kutoka utumwani Misri kwenda Kanaan mahali ambako ni umbali wa takribani Kilomita 600.

Unaweza kushangaa unaposoma au kuhadithiwa habari ya safari hiyo na ukajiuliza ilikuwaje wakatumia siku nyingi hivyo kusafiri katika umbali ambao leo hii mtu anaweza kutembea na akatumia muda usiozidi hata wiki mbili kufika mahali husika yenye umbali huo.

Hata hivyo, kulikuwa na sababu kwa Mungu kuwatembeza Wana wa Israel umbali huo mfupi kwa miaka mingi nayo ni kuonyesha kuwa mafanikio huwa hayapatikani kirahisi na ili uyapate ni lazima upite katika vikwazo, changamoto na misukosuko ambayo itakupa kumbukumbu nzuri pale utakapokuwa unafaidi mafanikio yako.

Hadithi hii ya ugumu wa safari ya Wana wa Israel kuifikia Kanaan inaweza kufanana na safari nzito ambayo iko mbele ya Simba katika harakati zake za kumaliza msimu wa 2024/2025 kwa heshima kubwa na historia ya kipekee ya kutwaa mataji matatu kama ilivyo ndoto ya mashabiki, wapenzi, wamachama, viongozi na wachezaji wa klabu hiyo.

Baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuachia ratiba mpya ya kumalizia msimu wa 2024/2025, Simba italazimika kupita katika siku 49 ya kucheza mechi 10 ngumu za ndani na nje ya nchi ili itimize ndoto yake ya kutwaa mataji matatu, mawili yakiwa ni mashindano ya ndani na moja la kimataifa.


Sita za kibabe

Kati ya mechi hizo 10 ambazo Simba itacheza ndani ya siku 49, Simba inaweza kuwa na mechi sita za kujirudiarudia na zilizopangwa ndani ya muda mfupi dhidi ya timu tatu.

Kwa kuanzia itakuwa na mechi mbili za fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco ambazo zitachezwa ndani ya muda wa siku saba tu.

Mchezo wa kwanza utakuwa huko ugenini, Berkane, Morocco ambako Simba itakaribishwa na RS Berkane katika mechi iliyopangwa kuchezwa Mei 17, 2025 na timu hizo zitarudiana hapa Dar es Salaam Mei 25, 2025.

Simba ina mchi nyingine mbili zilizokaribiana dhidi ya timu moja ambazo ni dhidi ya Singida Black Stars, mmoja ukiwa ni wa Ligi Kuu na mwingine wa Kombe la Shirikisho la CRDB hatua ya nusu fainali.

Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo ni wa Ligi Kuu ambao umepangwa kuchezwa Mei 28, siku tatu baada ya Simba kumaliza mechi ya pili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Siku tatu baada ya timu hizo kucheza katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Simba na Singida Black Stars zitakutana tena Mei 31, 2025 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB utakaochezwa katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.

Simba pia inaweza kukutana na Yanga katika mechi mbili ndani ya muda mfupi ambapo mchezo wa kwanza ni wa Ligi Kuu baina yao uliopangwa kuchezwa Juni 15 na iwapo timu hizo zitakutana katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, kati ya Juni 26 hadi 28 mwaka huu, siku zisizozidi 13 baada ya miamba hiyo kukutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu.


 Mechi 10, miji sita

Mechi hizo 10 ambazo zimeshikilia hatima ya Simba kuondoka na mataji matatu msimu huu zitailazimisha timu hiyo kusafiri na kucheza katika miji sita tofauti nja na ndani ya Tanzania


1. Simba vs Pamba- Uwanja KMC Complex (Dar es Salaam)-08.05.2025

2.KMC vs Simba- Uwanja Ali Hassan Mwinyi (Tabora)-11.05.2025

3.RS Berkane vs Simba-Uwanja Berkane (Morocco)- 17.05.2025

4. Simba vs RS Berkane- Uwanja Benjamin Mkapa (Dar es Salaam)- 25.05.2025

5. Simba vs Singida Black Stars-Uwanja KMC Complex (Dar es Salaam)- 28.05.2025

6. Simba vs Singida Black Stars-Uwanja Tanzanite Kwaraa (Manyara)- 31.05.2025

7.Yanga vs Simba- Benjamin Mkapa (Dar es Salaam)- 15.06.2025

8.Kengold vs Simba- (Uwanja haujapangwa)- 18.06.2025

9. Simba vs Kagera Sugar- Uwanja Benjamin Mkapa (Dar es Salaam)- 22.06.2025

10. Fainali Kombe la Shirikisho la CRDB- Uwanja haujapangwa- Juni 26-Juni 28, 2025

Kocha wa Simba, Fadlu Davids amesema kuwa wanafahamu wana ratiba ngumu lakini watapambana kuhakikisha wanaikabili.

"Sio jambo rahisi kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi lakini ndio ratiba iko hivyo na tunalazimika kufanya mabadiliko ya wachezaji ili kutoa nafasi ya kupumzika na kutowachosha ili tuweze kuendana na changamoto iliyo mbele yetu.

"Jambo la msingi ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi hizo ili tuweze kumaliza vyema msimu," amesema Davids.

Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' amesema wako tayari kucheza mechi zilizobakia.

"Mechi ni nyingi na tunacheza katika muda mfupi lakini sisi ni kama askari muda wote tunapaswa kuingia uwanjani na kucheza," amesema Tshabalala