Kisa Awesu, KMC waidai Simba Sh200 milioni
Muktasari:
- Uongozi wa KMC umeeleza kuwa unahitaji Sh200 milioni kutoka Simba ili kumruhusu kiungo Awesu Awesu ambaye Simba imemsajili kimakosa kuendelea kuwatumikia.
Dar es Salaam. Uongozi wa KMC unataka kulipwa kiasi cha Sh200 milioni ili umuachie kiungo Awesu Awesu aitumikie Simba msimu ujao ikidai bado ni mchezaji halali wa klabu yao na Simba imemchukua kimakosa.
Mwanasheria wa KMC ambaye ni mjumbe wa bodi ya klabu hiyo, Cheaf Said alisema kuwa Simba ilipaswa kuwafuata mezani na kukubaliana kuhusu mchezaji huyo.
Cheaf amesema hayo muda mfupi baada ya kutoka katika kikao cha kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kilichoketi leo Agosti 10 katika makao makuu ya shirikisho hilo, Karume, Dar es Salaam.
"Ni kweli Awesu aliomba kuvunja mkataba akiwa na sababu kuwa anaenda kukuza kipaji sehemu nyingine barua hiyo aliandika Julai 10 na siku ya pili tulikaa naye kikao tukamwambia hatujakubali.
"Sababu ya kumkatalia ni sababu alizoleta kwaajili ya kuvunja mkataba alitakiwa kufanya ivyo kama timu imeshuka daraja au imeshindwa kumpa mahitaji yake hicho kitu kwake hakipo ni wazi kuwa amerubuniwa wa Simba ambayo inasema kuwa imemsajili akiwa mchezaji huru," amesema Cheaf.
Cheaf alisema Awesu bado ni mchezaji wao na leseni yake inasoma kwenye timu yao na Simba ambao wanasema ni mchezaji wao waliwafuata siku mbili kabla ya Mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kuomba kibari ili acheze wamewakatalia.
"Kama wamemsajili mchezaji huru kwetu walifuata Nini msimamo wetu ni Awesu kurudi KMC na kama Simba wapo tayari kulipa kiasi cha Sh200 milioni tunawaachia,
"Awali makubaliano yetu yalikuea ni Simba watulipe Sh70 milioni walikwama kwa sababu walikuwa na Sh60 milioni sasa kutokana na usumbufu walio tupa tunatama Sh200 milioni.
Alisema kitendo walichokifanya Simba ni makosa kimpira kwani wamemshawishi mchezaji ambaye bado ana mkataba na KMC kwa kumpa fedha ili avunje mkataba bila kufuata sheria.
Simba yafunguka
Mwanasheria wa Simba, Hosea Chamba amesema wanasubiri hukumu kutoka kamati ya sheria na hadhi ya wachezaji juu ya wachezaji wao, Awesu Awesu na Valentino Mashaka huku akikiri kuwa hawahusiki juu ya shtaka linalomuhusu Yusuf Kagoma.
Chamba amesema Simba imeshtakiwa na Geita Gold pamoja na KMC juu ya wachezaji wao Awesu na Mashaka hawana shitaka kutoka kwa watani zao Yanga juu ya Kagoma wao wamemnunua mchezaji huyo kutoka Singida Fountaine Gate.
“Awesu na Mashaka sisi tumewasajili wakiwa wachezaji huru hivyo uwepo wa kesi kutoka timu hizo mbili tunasubiri hatma zake kutoka Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji,” amesema na kuongeza;
“Kuhusu Kagoma hakuna kesi kati yetu na Yanga na ndio maana alikuwa na mwanasheria wake na mimi nilikuwa nawasimamia Awesu na Mashaka huyo Kagoma ni mchezaji wetu halali.”