Prime
Siku iliyokuwa inasubiriwa imefika

Ile siku ndio kesho. Kilele cha wiki ya Simba kitafanyika Wanasimba zaidi ya 60,000 watakutana Uwanja wa Benjamin Mkapa kukamilisha vaibu lao la kuukaribisha msimu mpya chini ya kauli mbiu yao ya Ubaya Ubwela.
Ndio siku ya furaha zaidi kwa mashabiki na wanachama wa Simba. Saa chache zijazo wanakwenda kushuhudia furaha mpya baada ya kupitia miezi kadhaa ya machungu na karaha za kutoona ladha ya pira biriani waliyoizoea.
Ukiachana na mengine yote shauku ya Wanasimba kesho ni kushuhudia usajili mpya. Unafananaje? Hawataki kuhadithiwa maana katika karata waliyoicheza viongozi ni kuficha kabisa mechi za maandalizi wakiwa kambini Misri zisionekana laivu mpaka walipomaliza na jana waliwaonjesha waandishi kidogo kuona wachezaji wao wanafananaje.
Lakini vilevile mashabiki wanataka kuona kikosi chao cha kwanza kinafananaje? Nani anafanya nini? Ingawa za ndani ni kwamba mastaa wengi wapya huenda wasijiachie sana na watatumika muda mfupi kuficha silaha za mechi ya dabi Agosti 8 kwa kuwa imekaa vibaya.
Hata umoja wa vigogo na kurejea kwenye usukani wa mambo kwa tajiri Mohammed Dewji kumeongeza hamasa kwa mashabiki hao pamoja na watani wao kupata shauku ya kuona inakuwaje, wamejipangaje? Ingawa hata kauli mbiu ya ubwaya ubwela imekuwa na msisimko wa aina yake na kufanya mashabiki kulihodhi tamasha lao.
Mageti ya Uwanja wa Benjamin Mkapa yatakuwa wazi kuanzia saa 3:00 asubuhi kuwaruhusu mashabiki waliokata tiketi ambazo zilimalizika siku tatu kabla kuanza kuingia huku wengi wakionekana kujivunia zaidi uzi wao mpya ambao safari hii umetoka mapema zaidi ya kipindi cha nyuma hivyo kufanya wengi kuchukulia kama mtoko wao.
Mashabiki tangu juzi walianza kutamba baada ya kutangaziwa tiketi za tamasha hilo zimemalizika, pamoja na yote kikubwa kinachowapeleka uwanjani kesho ni kupata kiburi cha kuwatambia watani zao Yanga kutokana na kile watakachoshuhudia ndani ya dakika 90 na wanataka kuweka pia rekodi ya kuujaza uwanja mapema kwani Wikiendi hii ni Mwananchi Day pia.
NDANI YA UWANJA
Hapa ndio patamu. Ubwaya Ubwela ndio uko hapa kuanzia saa 1:30 usiku. Kocha mpya Fadlu Davids kwa mara ya kwanza mbele ya Wanasimba ataupanga mziki wake kukiwasha na APR ya Rwanda.
Simba chini ya Fadlu haijaonekana ikicheza uwanjani hata kwa dakika moja ambapo mechi zao za kirafiki ilizocheza ilipokuwa kambini jijini Ismailia nchini Misri hazikuonyeshwa kokote na kuwafanya mashabiki wa wekundu hao kuwa na kiu kubwa.
APR ambao ni kaimu bingwa wa Kombe la Kagame ndio watakuwa kipimo Cha kwanza kwa Simba tangu itue nchini, ukiacha zile ambazo wekundu hao imezicheza Misri na kushinda zote. Tukutane kwa Mkapa. Ubaya Ubwela.
MACHO KWA HAWA
Simba imefanya usajili wa wachezaji wengi zaidi msimu huu tofauti na misimu kadhaa iliyopita na mashabiki wa timu hiyo watataka zaidi kuwaona Karaboue Chamou, Joshua Mutale, Omary Omary, Charles Ahoua, Steven Mukwala, Abdulrazak Hamza, Debora Mavambo, Yusuf Kagoma, Kelvin Kijili, Awesu Awesu, Augustine Okajepha, Valentino Mashaka na Valentin Nouma.
Hapa ndiyo kutakuwa na gumzo kubwa la mashabiki, siyo wa Simba tu hadi wale wa Yanga na timu nyingine za Ligi Kuu Bara baada ya dakika 90 za mechi, kila mtu atakuwa na lake la kusema.
INGIZO JIPYA
Jana Simba ilimtambulisha kipa mpya wa timu hiyo, Moussa Camara 'Spider' kwa mkataba wa miaka miwili akitokea AC Horoya ya Guinea.
Camara ni maarufu kwa jina la Spiderman, kwa umahiri wake wa kudaka mipira, ni raia wa Guinea mwenye umri wa miaka 25 amejiunga na klabu hiyo ya Msimbazi ili kuongeza nguvu katika eneo hilo baada ya Ayoub Lakred kuumia akiwa kambini jijini Ismailia, Misri.
Baada ya kusaini mkataba, kipa huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Guinea amesema anaushukuru uongozi wa Simba kwa kumpa nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha Mnyama.
Taarifa zinasema kuwa leo atapata muda mchache wa kuwaonyesha mashabiki makali yake, lakini ubora wake wa juu utaonekana Agosti 8 akiwa ameshazoeana na wenzake.
SAPRAIZI YA AHMED ALLY
Achana na kauli mbiu aliyoibuni ya Ubwaya Ubwela ambayo imeshika kasi. Leo mashabiki wanashauku ya kuona anakujaje? Amejipangaje? Kwani ndiye kiongozi aliyekuwa akiwahamasisha tangu msimu umalizike. Tamasha lililopita Ahmed aliingia uwanjani akiwa na ngamia kisha akavutia kwa ile "Wanathiiimbaaaaa" iliyoteka vibaya.
Safari hii acha tusubiri kuona ataingiaje.
Utamu zaidi wa tamasha hilo utakuwa ni utambulisho wa wachezaji watakaoiwakilisha Simba kuelekea msimu ujao ikiwa na mastaa wapya 12 waliosajiliwa dirisha hili.
Kitu ambacho kitavutia wengi kwenye utambulisho huu wa wachezaji ni namna Msemaji wa klabu hiyo Ahmed Ally atatumia maneno ya mbwembwe na yenye kukera kuwatambulisha.
Inaelezwa pia baadhi ya wachezaji wa Simba nao watakuwa na mbwembwe zao kwenye kuingia ndani ya uwanja katika utambulisho huo.
BURUDANI MUZIKI
Ndani ya tamasha hilo kutakuwa na burudani mbalimbali za muziki ambapo kuna wasanii wasiopungua sita ambao watafanya shoo kali kwenye jukwaa.
Yumo Joh Makini 'Mwamba wa Kaskazini, Chino Wana Man, Ally Kiba huku Tundaman alitarajiwa kuthibitishwa jana mchana kuwa sehemu ya watakaotoa burudani.
Msanii Dulla Makabila Simba imemuondoa jina lake kabisa kutokuwa sehemu ya watakaotoa burudani ikielezwa mashabiki wengi wa wekundu hao kumkataa kwa kuwahi kuisema vibaya timu yao.
FADLU ATOA NENO
Kocha mpya wa Simba, Fadlu Davis, amesema timu yake ipo vizuri lakini anaamini baada ya wiki tatu zaidi, basi mziki wake utakuwa tayari ingawa wachezaji waliosajiliwa wapo kwenye kiwango cha juu sana.
“Kwanza kabisa nipongeze mfumo wa usajili, bodi ya klabu na rais kwa usajili. Nadhani tumesajili kikosi kizuri, cha umri mdogo na chenye nishati. Kikosi ambacho kina wachezaji 14 wapya wakiungana na wengine 14 waliokuwepo.
“Ni wachezaji wenye vipaji vizuri na wana kitu cha kuonyesha watakuwa wachezaji wakubwa kwa klabu. Hiyo ndiyo maana ya balansi ya kikosi, kuna sehemu chache ambazo tunaziangalia lakini tuna balansi nzuri," alisema.
APR YA HITIMANA
Kocha mkuu wa APR ya Rwanda, Thierry Hitimana alisema; "Sijaiona Simba yenye wachezaji wapya, kulingana na maandalizi yao ya msimu mpya, waliyoyafanya nchini Misri, ina kocha mpya, hivyo hautakuwa mchezo mwepesi, nautarajia utakuwa wa kimbinu zaidi."
"Ukiachana na hilo, Simba ni klabu kubwa, kitakuwa kipimo kizuri kwetu, kujiandaa na mashindano mbalimbali yaliopo mbele yetu kama Ligi ya Mabingwa Afrika,"alisema Hitimana kocha msaidizi wa zamani wa Simba chini ya Didier Gomes.
APR kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, hatua ya awali itakutana na Azam FC, jambo ambalo kocha Hitimana alisema; "Kucheza na Simba itatusaidia zaidi, kwani ina wachezaji ambao wana ushindani wa kimataifa, kulingana na usajili walioufanya."
Kumbuka APR ilimaliza nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika hivi karibuni hapa nchini.