Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinachowabeba Yanga kwa Waangola, Singida BS haina presha

Muktasari:

  • Katika mechi za kwanza ugenini, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wiliete huko Angola huku Singida Black Stars ikipata ushindi wa bao 1-0 huko Rwanda dhidi ya Rayon Sports na Mlandege ilifungwa mabao 2-0 na Ethiopian Insurance ya Ethiopia.

Dar es Salaam. Yanga inaikabili Wiliete ya Angola katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni, Dar es Salaam huku ikiwa na historia nzuri dhidi ya timu kutoka Angola.

Mara mbili tofauti ambazo Yanga imewahi kukutana na klabu za Angola miaka ya nyuma, ilisonga mbele na haikupoteza mechi ya nyumbani.

Historia inaonyesha mwaka 2007, Yanga ilicheza dhidi ya Petro De Luanda katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2. Mchezo wa kwanza ugenini ilifungwa mabao 2-0, nyumbani ikashinda 3-0.

Pia mwaka 2016, Yanga ilicheza dhidi ya Sagrada Esperansa na kuitoa kwa jumla ya mabao 2-1 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Mechi ya nyumbani ilishinda mabao 2-0, ugenini ikapoteza kwa bao 1-0.

Kocha wa Yanga, Romain Folz amesema kuwa wanataka kuhakikisha wanaimalizia vyema kazi nzuri ambayo wameianza vizuri ugenini.

"Tulifanya kazi nzuri kupunguza ubora wa wapinzani wetu ugenini. Maandalizi yameenda vizuri na naamini tutatoa kilicho bora katika mchezo wa kesho (leo). Unapocheza katika Ligi na Mashindano ya CAF, inakupa kiwango kimoja cha umakini na kujitolea dhidi ya mpinzani unapocheza naye nyumbani au ugenini.

"Nilichokisema kwa wachezaji wangu ni kwamba huu mchezo wanapaswa kutoa zaidi ya kile walichokitoa katika mchezo wa kwanza. Wapinzani wetu hawana cha kupoteza. Mechi ya kwanza imeshapita na nawaambia wachezaji wangu waachane na matokeo ya mechi iliyopita na wacheze kama mechi ya kwanza ilikuwa 0-0," amesema Folz.

Baada ya mchezo huo, kuanzia saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kutakuwa na mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Singida Black Stars dhidi ya Rayon Sports.

Ushindi wa bao 1-0 ambao Singida Black Stars iliupata ugenini huko Rwanda, unailazimisha leo kuhakikisha inapata ushindi au sare ya aina yoyote ili iweze kuingia raundi ya pili ya mashindano hayo.

Mtendaji Mkuu wa Singida Black Stars, Jonathan Kasano ametamba kuwa maandalizi yao ni mazuri na wana imani wataitupa nje Rayon.

"Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hii. Tunawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi katika Uwanja wa Azam Complex ili kutupa sapoti na hatutowaangusha," amesema Kasano.

Katika Uwanja wa New Amaan Complex, wawakilishi wengine wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Mlandege watakuwa na kibarua cha kupindua matokeo ya kichapo cha mabao 2-0 walichokipata katika mechi ya kwanza ugenini huko Ethiopia dhidi ya Ethiopia Insurance.

Mchezo huo wa Mlandege umepangwa kuanza saa 10:15 jioni