Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibailo: Beki Namungo anayetaka ubunge

Malengo ni hatua fulani katika maisha ya mtu ambayo hajaifikia na anatarajia kuifikia na katika maisha ya kawaida kila mwanadamu ana malengo yake.

Jambo la msingi ni muhimu kufahamu lengo lako vizuri ambalo unatakiwa kulifikia, kama ambavyo anafunguka beki wa Namungo Hassan Kibailo kuwa ana ndoto siku moja kuwa kiongozi wa kisiasa.

Mwananchi limefanya mahojiano na beki huyo ambaye amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ndoto yake ya kuja kuliongoza jimbo la Ibungilo lililopo Jijini Mwanza na namna alivyoingia kwenye soka la ushindani akitokea mtaani.


Kufuata nyayo za Majaliwa

Ili ndoto iweze kutimia lazima uwe na mtu ambaye umekuwa ukijifunza vitu kutoka kwake ama ndiyo kioo chako kama ambavyo Kibailo ameweka wazi kuwa amekuwa akijifunza na kumtazama Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

"Nina ndoto ya kuwa Mwanasiasa, Mbunge na nimekuwa nikimtazama zaidi Waziri Mkuu ambaye pia ni boss wangu Kassim Majaliwa  ni kiongozi ambaye anaishi vizuri na watu hakuna anayemchukia.

"Nimekuwa nikijifunza mengi kupitia yeye ni kiongozi muadilifu na ili uweze kuwa bora unatakiwa kuishi na watu vizuri, kuwa mfano wa kuigwa lakini pia kuweza kuongoza jamii nzima inayokuzunguka.

"Mwanza nina jimbo langu pale kuna sehemu inaitwa Ibungilo nafahamika sana na wamekuwa wakinipa ushirikiano namshukuru Mungu hadi hapa nilipofikia kuna watu nyuma yangu kutoka katika jimbo hilo ambalo jina langu maarufu ambalo wamekuwa wakiniita ni Hassan Poti,"

Anasema anasifa zote za kuweza kuwaongoza watu kwasasa anajipanga lakini kuhusiana na sifa anazo kwasababu anajua kusoma na kuandika huku akiweka wazi kuwa ana elimu ya kidato cha nne.


Mtaa umempeleka Pamba

Kibailo ni mtoto wa mtaani na soka lake amelianzia huko huko katika timu ya Pasias Boys ‘Juma Kampong’ ya jiji Mwanza na baada ya hapo alikwenda katika akademi ya TSC na ndipo safari yake ya soka ikaanza.

Beki huyo anasema walipata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa watoto wa mtaani na walichukua ubingwa wakiwa nchini Brazil na hapo ndio maisha yake ya soka yalipoanzia.

“Niliporudi nilicheza Pamba na timu ikaingia kwenye hatua ya 'Play Off' ndipo Coastal Union waliniona na kuvutiwa na huduma yangu baada ya hapo basi nikasaini.

“Nilikuwa mtu wa mazoezi sana nikiwa na Coastal Union, nilipata nafasi ya kucheza nikaonyesha nilichokuwa nacho na timu zingine zikaniona hivyo mkataba wangu ulivyoisha nikaamua kuondoka kwenda kutafuta changamoto nyingine.”


Goti lilimzuia kwenda Simba

Kibailo anasema baada ya kuondoka Coastal alipokea ofa ya Mtibwa Sugur lakini akiwa na timu hiyo alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kupata majeraha ya goti yaliyomweka nje ya uwanja muda mrefu.

“Baada ya kusajiliwa Mtibwa sikuweza kudumu kwa muda sababu nilipofika sikuwa na msimu mzuri nilipata majeraha ya kuniweka nje kwa muda mrefu, mkataba wangu ulipoisha niliachana nao na kurudi Mwanza kujiweka vizuri kwa sababu mtaji wa kweli kwetu sisi wachezaji ni afya.

“Kuna vitu vingine vilitokea lakini havina afya kuvizungumzia, kikubwa nilipona baada ya kujitibia na nikawa nafanya mazoezi mwenyewe mdogo mdogo hadi nikakaa sawa kabisa."

Anasema alikaa nje ya uwanja mwaka mmoja na zaidi alilichukulia kama changamoto lakini kutokana na uwezo aliokuwa nao hakuchukua muda kurudi uwanjani hadi sasa anaipambania Namungo.

"Ubora niliokuwa nao nakumbuka nilipata ofa kutoka Simba na Yanga lakini kipindi hicho nilikuwa tayari nimepata shida ya goti, ndoto ya kwenda timu hizo ilishindikana lakini naamini nikipata nafasi naweza kufanya vizuri."


Ishu ya Kapombe, Mwenda

Kibailo anasema kwa sababu yeye anacheza beki wa kulia basi beki ambaye anamvutia kwa Ulaya ni Dan Alves ambaye aliwahi kutamba katika klabu ya Barcelona na timu ya Taifa ya Brazil kwa soka la ndani anavutiwa na mkongwe Shomari Kapombe na Israel Mwenda.

"Navutiwa na wachezaji wengi lakini bora ni Kapombe, Mwenda ni mabeki ambao nimekuwa nikiwatazama na kujifunza vitu kutoka kwao ni wachezaji wazuri na mfano wa kuigwa kutokana na namna wanavyopambana."

Beki huyo anasema anavutiwa na Alves kutokana na uwezo wake mkubwa kwenye ukabaji sambamba na kupeleka mashambulizi hali ambayo inawapa tabu wapinzani.

“Nje bwana yule Dan Alves anavyocheza anakaba na kushambulia na burudani anakupa kwa hiyo navutiwa naye sana, napenda anavyocheza na kuna wakati namuangalia na kuchukua baadhi ya vitu ili niwe kama yeye au zaidi,”anasema Kibailo.


Aiwazia Taifa Stars

Kibailo baada ya kucheza timu ya taifa kwa watoto wa mtaani sasa anasema akili yake ameigeuzia kupata nafasi ya kucheza katika timu kubwa ya Taifa.

“Siri yangu ya mafanikio ni kujituma na mpira ni mchezo wa wazi na watu wataona, kikubwa kazi kamwe usimuache Mungu kwa sababu yeye ndio mpaji,”anasema na kuongeza;

“Muda wowote na wakati wowote nitakuwa kwenye timu ya Taifa kwa sababu ni ndoto ambayo inaninyima usingizi sana, kwenye soka nilichojifunza ni kutakiwa kuthamini muda.” alisema beki huyo anayecheza kikosi cha kwanza Namungo.