Kocha Bilibao aipa onyo Man United

Muktasari:
- Athletic Bilibao itaikaribisha Man United, Mei Mosi mwaka huu katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Europa League.
Kocha wa Athletic Bilibao, Ernesto Valverde ametuma ujumbe wa kuionya Man United ikiwa zimebaki siku chache kabla timu hizo kukutana kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Europa League.
Valverde ameyasema hayo juzi, Jumatano, Aprili 23 baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Las Palmas katika muendelezo wa Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’.

Kocha huyo amesema kwamba wana malengo mawili mbele yao kabla ya kukamilisha msimu.
“Tupo kwenye mashindano ya Europa League, lengo letu tunahitaji kufika fainali pia kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.
“Timu yetu ipo vizuri na ndiyo maana tunahitaji kufika fainali ya Europa na tunajiamini katika hilo”, amesema Valverde.

Hadi sasa Bilibao imecheza michezo 33, imeshinda mechi 16, sare mechi 12 huku ikipoteza mechi tano ambapo inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa La Ligi ikiwa na pointi 60.
Katika michuano ya Europa, Bilibao iliitoa AS Roma katika hatua ya 16 bora baada ya kupindua matokeo kwa kupata ushindi wa mabao 3-1 kwenye uwanja wa nyumbani kwani katika mchezo wa ugenini ilipoteza kwa mabao 2-1.

Katika hatua ya robo fainali ilifanikiwa kusonga mbele baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 2-0 dhidi ya Rangers kwani katika mchezo wa ugenini ilitoka suluhu.

Manchester United imekuwa na muendelezo mbaya kwenye Ligi Kuu msimu huu kwani imecheza mechi 33 ambapo imeshinda mechi 10, imepata sare mechi nane na kupoteza mechi 15 huku ikishika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
United ambayo imetoka kuonyesha maajabu ya kupindua meza dhidi ya Lyon baada ya kutoka nyuma na kushinda mabao 5-4 kwenye mchezo uliopita ni dhahiri kabisa timu hiyo yenye mashabiki wengi ulimwenguni inahitaji kufika fainali ili kuhakikisha wanarudi kwenye mashindano ya Ulaya msimu ujao.

Iwapo Man United itafanikiwa kwenda fainali itarejea tena kwenye uwanja wa San Mames ambao utatumika kwenye mchezo wa fainali May 21 mwaka huu huku kwa upande wa Athletic Bilibao huenda wakacheza mchezo wa fainali kwenye uwanja wao wa nyumbani endapo wataitoa Man United.