Hii hapa Safari ya Simba kimataifa

Aprili 27 mwaka huu, Simba iliandika historia ya kuingia kwa mara ya kwanza katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana na Stellenbosch ya Afrika Kusini ugenini.
Sare hiyo katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Durban iliifanya Simba isonge mbele ikibebwa na ushindi wa bao 1-0 ilioupata katika mechi ya kwanza nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Aprili 20.
Lakini pia imekuwa ni mara ya pili kwa Simba kuingia hatua ya fainali ya mashindano ya Klabu Afrika ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 1993 ilipotinga hatua hiyo katika Kombe la CAF ambalo mwaka 2004 liliunganishwa na Kombe la Washindi kupata Kombe la Shirikisho Afrika.
NJIA NGUMU NDIO SAHIHI
Huwezi kuwa bora kama haushindani na walio bora na hilo limejidhihirisha katika safari ya Simba kuanzia raundi ya kwanza hadi ilipojihakikishia tiketi ya fainali.
Wawakilishi hao wa Tanzania wameruka viunzi vingi vigumu hadi wakafanikiwa kufika katika hatua hiyo ambayo ni ya juu zaidi katika mashindano ya klabu Afrika.

Simba haikuanzia katika hatua ya awali kutokana na kuwa katika nafasi bora kwenye chati ya viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Katika raundi ya kwanza ilipangwa kucheza na Al Ahli Tripoli ya Libya ambapo mechi ya kwanza ugenini, matokeo yalikuwa ni sare tasa na ziliporudiana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba ikaibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Wakati inakutana na Simba, Al Ahli Tripoli ilikuwa katika nafasi ya 33 katika chati ya ubora ya CAF huku ikibebwa na uzoefu na mafanikio makubwa iliyoyapata katika mashindano ya klabu Afrika.
Timu hiyo ya Libya imewahi kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja ambayo ni mwaka 2022 lakini pia imewahi kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja mwaka 2017.

Baada ya kuitoa Al Ahli Tripoli, Simba ilipangwa katika kundi A la mashindano hayo ikiwa sambamba na timu za CS Constantine ya Algeria, CS Sfaxien ya Tunisia na Onze Bravos Marquis ya Angola.
Simba ilimaliza ikiwa kinara wa kundi hilo baada ya kukusanya pointi 13 katika mechi sita, ikiibuka na ushindi mara nne, kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja ambapo ilifunga mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.
Ilianza kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bravos do Maquis nyumbani, ikafungwa mabao 2-1 ugenini na CS Constantine kisha mchezo uliofuata ikapata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya CS Sfaxien.
Ilienda kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya CS Sfaxien, kisha ikatoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Bravos do Maquis na ikamalizia kwa ushindi wa nyumbani wa mabao 2-0 dhidi ya CS Constantine.
Katika kundi hilo, ni Bravos pekee ambayo haikuwa na uzoefu mkubwa na mashindano ya klabu Afrika au kuwa katika nafasi kwenye chati ya CAF ya ubora wa klabu tofauti na ilivyokuwa kwa CS Sfaxien na CS Constantine.
Sfaxien imewahi kuchukua taji la Shirikisho Afrika mara tatu huku pia ikiwa imewahi kutwaa ubingwa wa Kombe la CAF mwaka 1998 na hadi makundi hayo yanapangwa ilikuwa katika nafasi ya 39 katika chati ya ubora ya klabu ya CAF na Constantine msimu wa 2018/2019 ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Al Masry ya Misri ndio ilikuwa mpinzani wa Simba kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya mechi mbili baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, mchezo wa kwanza huko Misri, Al Masry ilipata ushindi wa mabao 2-0 na Simba ikapata ushindi kama huo ilipocheza hapa Dar es Salaam.
Timu hiyo ya Misri iliingia katika hatua ya robo fainali ikiwa nafasi ya 38 kwenye chati ya ubora Afrika huku ikiwa na historia ya kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja ambayo ilikuwa ni mwaka 2018.
Kwenye hatua ya nusu fainali ndio Simba ikakutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini ambayo ingawa haikuwa na uzoefu wa mashindano hayo, iliingia katika hatua hiyo kwa kuitoa Zamalek iliyokuwa bingwa mtetezi wa Kombe la Shirikisho Afrika.
NAMBA HAZIPINGWI
Simba haijafika kinyonge katika hatua ya fainali na hilo linathibitishwa na takwimu bora ambazo yenyewe na baadhi ya wachezaji wake mmojammoja wameziweka hadi inaingia katika hatua hiyo.

Simba inashika nafasi ya pili katika chati ya timu zinazofanya vizuri kwa kumiliki mpira kwenye mashindano hayo msimu huu ikiwa na wastani wa kutawala mchezo kwa asilimia 57.6.
Timu hiyo inashika nafasi ya pili katika chati ya timu zilizocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao (clean sheet) ambapo imefanya hivyo katika michezo sita huku kinara ikiwa ni RS Berkane ambayo imecheza mechi nane bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Nafasi ya pili katika chati ya timu zilizotengeneza nafasi nyingi inashikiliwa na Simba ambapo inazo 24 na inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya kona ikiwa nazo 63 na ndio timu kinara katika orodha ya timu zilizogusa mara nyingi mpira katika lango la timu pinzani ambapo imefanya hivyo mara 223.
Kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua anashika nafasi ya tatu katika chati ya nyota wanaoongoza kwa kuhusika na idadi kubwa ya mabao kwenye kombe hilo ambapo amehusika na mabao matano, akifunga matatu na pia kutoa asisti mbili za mabao.
Ahoua anaongoza chati ya wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi kwenye mashindano hayo akiwa nazo 27 huku akishika nafasi ya pili katika chati ya nyota waliotengeneza nafasi kubwa za mabao akiwa nazo tano.
Kipa Moussa Camara anashika nafasi ya pili kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa ambapo amefanya hivyo katika michezo sita.
Elie Mpanzu anashika nafasi ya pili katika chati ya wachezaji wanaoongoza kwa kukokota mpira ambapo ana wastani wa kufanya hivyo mara 3.7 kwa mchezo na Kibu Denis ana wastani wa kufanya hivyo mara 3.4 kwa mechi.