Hemed Morocco na penalti ya Terry CHAN
Muktasari:
Tanzania imewahi kushiriki CHAN Mara mbili na zote iliishia katika hatua ya makundi mara ya kwanza ikiwa ni 2009 na mara ya pili ni 2020.
Usiku wa Mei 21, 2008 ulikuwa na maana kubwa kwa beki na nahodha wa Chelsea, John Terry pale Moscow, Russia katika Uwanja wa Luzhniki.
Ilikuwa ni dhidi ya Manchester United katika Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Terry mbele ya kipa Edwin Van Der Sar alikuwa na fursa ya kuibuka shujaa kwa timu yake iwapo angefunga mkwaju wa penalti ambayo ulikuwa wa tano kwa Chelsea baada ya kupata nne.
Katika penalti tano za kwanza, Man United tayari ilikosa moja ya Cristiano Ronaldo huku nyingine nne zikifungwa na Carlos Tevez, Michael Carrick, Owen Hargreaves na Luis Nani huku Chelsea ikipata nne zake kupitia kwa Michael Ballack, Luciano Belleti, Frank Lampard na Ashley Cole hivyo kama Terry angefunga penalti ya mwisho, Chelsea ingetwaa ubingwa ambao ungekuwa wa kwanza kwa timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo Terry alikosa penalti hiyo na kufanya mwamuzi Lubos Michel kutoka Slovakia kuongeza penalti mojamoja ambapo Man United walifunga penalti ya saba kupitia kwa Ryan Giggs huku Nicholas Anelka akikosa kwa upande wa Chelsea na hivyo kufanya ubingwa huo uende jiji la Manchester.
Dunia na mashabiki wengi wa Chelsea hadi leo hii hawana habari na Anelka japo naye alikosa penalti na kidole kinanyooshwa kwa Terry kwa sababu yeye ndio alikuwa na nafasi ya kuipa timu ubingwa.
Ni wazi kwamba kama John Terry angepata, mambo yasingekuwa mengi na hata Chelsea isingefika penalti ya saba ambayo alipiga Anelka.
Nimekumbuka hadithi hii ya John Terry katika kipindi hiki ambacho timu yetu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ina kibarua mbele yake cha mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024 ambayo yanafunguliwa leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Bahati iliyoje ni kwamba mechi hiyo ya ufunguzi inahusisha Taifa Stars na Burkina Faso ambayo imepangwa kuanza saa 2:00 usiku.
Kwa kukumbushia tu, hizi Fainali za CHAN zilianza mwaka mmoja tu baada ya John Terry kukumbana na kadhia ya kukosa penalti iliyoinyima Chelsea fursa muhimu ya kuandika historia ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza kule Moscow.
Katika fainali hizi za CHAN 2024, Kocha wetu Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Selemani ‘Morocco’ anakutana na hadithi inayokaribia kufanana na penalti ile muhimu ya John Terry kwa Chelsea mwaka 2008.
Utofauti ni kwamba Morocco ni kocha na hawezi kupiga penalti kulinganisha na Terry lakini kwa utafsiri wa matukio yao kubeba hatima sio vibaya kuwahusianisha.
Wakati kipindi kile John Terry alikuwa na kibarua cha kuiwezesha Chelsea kutwaa ubingwa wa kwanza Ulaya, Morocco ana kibarua cha kuwa kocha wa kwanza kuivusha Taifa Stars kutoka hatua ya makundi kwenda za juu kwenye fainali tofauti za Afrika.
Katika Fainali za Mataifa Afrika (AFCON), Taifa Stars katika awamu tatu tofauti ilizoshiriki ilikomea katika makundi ikianzia fainali za 1980 kule Nigeria, kisha za 2019 Misri na za 2023 zilizofanyika Ivory Coast.
Kwenye Fainali za CHAN mara mbili tofauti hapo nyuma ambapo ilishiriki napo haikuweza kufika hata mtoano kwa maana ya fainali za 2009 nchini Ivory Coast na Fainali za 2020 kule Cameroon.
Kwa maana hiyo, Morocco ana penalti muhimu ya kutuondoa unyonge huu kama ambavyo Terry alikuwa nayo ya kuipa Chelsea Ufalme wa Ulaya, tuombe Mungu tu kocha wetu apate penalti yake na yasijitokeze ya nahodha wa zamani wa Chelsea.
Lakini kama Morocco akifanikiwa na Taifa Stars katika CHAN, atasaidia kupunguza hisia hasi juu ya makocha wazawa ambayo wengi wamekuwa nayo kwamba bado hawastahili kupewa majukumu mazito ya kuinoa timu yetu ya taifa.
Tunapoianza CHAN, Morocco anapaswa kutambua kwamba amebeba dhamana kubwa ya makocha wazawa kama ambavyo Terry aliibeba ya mastaa wa Chelsea kipindi kile.
Kufanikiwa kwa Morocco kutakuwa ni nafuu kubwa kwa makocha wazawa na kuwapa nguvu ya kusimama mbele ya umma kutamba kuwa wanaweza kufanya kile ambacho wengi hawaaanini kwamba wanakiweza hivyo bado wanahitaji kuendelea kuaminiwa.
Lakini kama atashindwa, atazidi kuwapa nguvu wale ambao imani yao kwa makocha wazawa ni haba na itaendelea kutengeneza mazingira magumu kwa wazawa kupatiwa fursa kubwa za kuongoza mabenchi ya ufundi katika klabu zetu kubwa na Taifa Stars.
Morocco na wasaidizi wake wakumbuke kwamba mafanikio yakipatikana yatakuwa ya nchi nzima lakini mambo yakiwa tofauti, kundi kubwa la watu litarusha mishale kwao na watawaachia msalaba wao peke yao.
Bahati nzuri Morocco anaiongoza Taifa Stars katika CHAN 2024 akiwa amesharahisishiwa mambo kama ambavyo mazingira yalikuwa rahisi kwa Terry alipokuwa anaenda kupiga penalti ya mwisho usiku ule wa 2008 kule Russia.
Wakati Terry akienda kupiga penalti ya ushindi baada ya wenzake wanne kufunga za mwanzo huku wapinzani wao wakiwa wameshakosa moja, Morocco anaingia CHAN akiwa na uhakika wa sapoti kubwa kutoka kwa serikali, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na mashabiki wa soka nchini.
Timu ipo nyumbani hivyo itapata hamasa kubwa ya mchezaji wa 12 ambaye ni shabiki kulinganisha na timu pinzani.
Morocco anaingia CHAN huku akiwa na kikosi chenye wachezaji ambao wanatoka katika miongoni mwa ligi bora inayoshika nafasi ya nne barani Afrika.
Taifa Stars ya Hemed Morocco inaingia CHAN ikiwa na wachezaji kutoka Simba na Yanga ambao klabu zao zimewapa uzoefu na hali nzuri ya kujiamini kwa kushiriki hatua za juu za mashindano ya klabu Afrika na kwa uendelevu.
Kiufupi Morocco ndio kabaki na penalti ya ushindi. Afunge awe shujaa au akose ageuke John Terry katika usiku ule kwenye Uwanja wa Luzhniki.