Harambee Stars yaanza vyema CHAN 2024
Muktasari:
- Katika fainali hizo zilizofanyika Algeria na Senegal kutwaa ubingwa kwa kuifunga wenyeji kwa penalti 5-4, baada ya timu hizo kutoka suluhu (0-0), Congo haikufunga bao lolote, huku eneo la kujilinda likiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.
Timu ya Kenya, Harambee Stars, imeanza vyema Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya ndani (CHAN), baada ya kuwafunga mabingwa mara mbili, DR Congo bao 1-0, katika mechi ya kundi A iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kasarani, Kenya.
Bao la wenyeji, lilifungwa na nyota wa kikosi hicho, Austine Odhiambo anayeichezea Gor Mahia dakika ya 45, kwa ustadi mkubwa akiwatoka mabeki wa DR Congo, baada ya kupokea pasi iliyopigwa na mshambuliaji nyota wa timu hiyo, David Sakwa.
Pambano hili ni la nane kukutana ambapo Kenya ambalo ni taifa tofauti la 33, kushiriki michuano ya CHAN tangu ilipoanza rasmi mwaka 2009 kule Ivory Coast, imeshinda mara tatu tu na kuchapwa mechi nne, huku mara moja iliyobaki zikitoka sare.
Kenya inayofundishwa na Benni McCarthy raia wa Afrika Kusini, baada ya ushindi huu, itapambana na Angola Agosti 7, kisha kuikabili Morocco Agosti 10, huku ikihitimisha hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa kucheza na Zambia, Agosti 17, 2025
Kwa upande wa DR Congo ambao ni mabingwa mara mbili wa CHAN mwaka 2009 na 2016, imeendeleza rekodi mbovu ya kutokufunga bao, kwa sababu katika fainali zilizofanyika mwaka 2022, kule Algeria ilimaliza ikiwa mkiani huku ikiwa haijafunga bao.
Katika fainali hizo zilizofanyika Algeria na Senegal kutwaa ubingwa kwa kuifunga wenyeji kwa penalti 5-4, baada ya timu hizo kutoka suluhu (0-0), Congo haikufunga bao lolote, huku eneo la kujilinda likiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.
Kwenye kundi hilo, Senegal iliongoza na pointi sita, ikifuatiwa na Ivory Coast iliyoshika nafasi ya pili na pointi nne, sawa na Uganda iliyokuwa ya tatu zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, huku DR Congo ikiburuza mkia na pointi mbili.
Michuano hii ilianza rasmi mwaka 2009, kwa lengo la kukutanisha wachezaji wanaocheza Ligi za ndani, ambapo kwa mara ya kwanza ilifanyika Ivory Coast, kuanzia Februari 22 hadi Machi 8, 2009, huku DR Congo ikiibuka mabingwa wa mashindano.
DR Congo iliibuka mabingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuifunga Ghana mabao 2-0, yaliyofungwa na Alain Dioko Kaluyituka na Hugues Bedi Mbeza, ambapo kikosi hicho wakati huo kilikuwa kinafundishwa na Kocha, Santos Mutumbile.
Congo ilikuwa kundi B la michuano hiyo, ilimaliza nafasi ya pili na pointi zake nne, nyuma ya Ghana iliyoongoza ikiwa na pointi tano, huku Zimbabwe ikishika ya tatu na pointi tatu, wakati Libya iliburuza mkia kufuatia kukusanya pointi mbili.
Baada ya DR Congo kuchukua ubingwa mwaka 2009 kule Ivory Coast, kikosi hicho kikatwaa tena taji la mwaka 2016, likiwa ni la pili kwake katika michuano hiyo iliyofanyika Rwanda, kufuatia kuifunga Mali kwa mabao 3-0, kwenye mechi ya fainali.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa Februari 7, 2016, kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Amahoro, mabao hayo ya DR Congo yalifungwa na Meschak Elia aliyefunga mawili dakika ya 29 na 61, huku lingine likifungwa na Jonathan Bolingi dakika ya 73.
Kikosi hicho kilitwaa ubingwa huo kikiwa chini ya Kocha, Florent Ibenge atakayeiongoza Azam FC msimu wa 2025-2026, huku Meschak Elia anayeichezea BSC Young Boys ya Uswisi akiibuka kidedea na tuzo ya mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP).
Mbali na tuzo ya MVP, Meschak Elia aliibuka mfungaji bora sawa na Ahmed Akaichi (Tunisia) na Chisom Chikatara (Nigeria), ambao kila mmoja alifunga mabao manne, huku aliyekuwa nyota wa Coastal Union, Ley Matampi alishinda tuzo ya kipa bora.