Guinea yachochea upya utata wa ubingwa Afcon
Dar es Salaam. Shirikisho la Soka la Guinea limeibua upya mjadala mzito barani Afrika baada ya kuiandikia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likiitaka ipitie upya matokeo ya Kombe la Mataifa ya Afrika 1976, wakidai walinyimwa ubingwa huo kwa mazingira yenye utata.
Katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Ethiopia, Guinea ilikuwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco lililofungwa na Chérif Souleymane kabla ya tukio la kushangaza kutokea, ambapo wachezaji wa Morocco walitoka uwanjani kupinga maamuzi ya mwamuzi.
Waliporejea, Morocco ilisawazisha kupitia kwa Ahmed Makrouh dakika ya 86 na kufanya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.
Sare hiyo iliifanya Morocco kumaliza juu ya kundi la mwisho kwa pointi tano na kutwaa ubingwa, huku Guinea wakishika nafasi ya pili.
Hata hivyo, baada ya kupita zaidi ya miaka 40, Guinea inaamini kuwa haikutendewa haki na sasa inataka ukweli ujulikane.
Mvutano mpya wapata nguvu
Hatua ya Guinea imepata uzito kufuatia utata uliojitokeza kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, ambapo maamuzi ya waamuzi na uendeshaji wa mashindano yamekuwa yakikosolewa vikali.
Vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa Guinea inaitaka CAF kutumia vigezo na misingi ileile iliyotumika kushughulikia kesi za hivi karibuni ili kupitia upya tukio la mwaka 1976.
Endapo hatua hiyo itakubaliwa, inaweza kufungua milango ya kupitia upya matokeo ya kihistoria ya mashindano hayo.
Sadio Mané aibua hisia
Wakati mjadala huo ukiendelea, nyota wa Senegal, Sadio Mané, ameibuka na kauli nzito akieleza kukerwa kwake na hali ya soka la Afrika.
“Kilichotokea kimevuka mipaka. Huu sio mpira tunaoupigania wala Afrika tunayoiamini. Kuna rushwa nyingi sana katika mchezo wetu,” alisema Mané.
“Wachezaji tunajituma uwanjani, lakini maamuzi ya nje ndiyo yanaamua matokeo na mataji.”
Kauli yake imeibua mjadala mpana, wengi wakiona ni ishara ya kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji ndani ya mfumo wa soka la Afrika.
Achraf Hakimi azua taharuki
Kwa upande wake, beki nyota wa Morocco, Achraf Hakimi, amezua mshangao baada ya kutangaza hadharani kuwa hatambui ushindi wa AFCON 2025.
“Mama yangu alinishauri nikatae kombe la AFCON, na nimeamua kufanya hivyo. Sikushinda mashindano hayo,” alisema Hakimi.
“Senegal walistahili ushindi. Si haki kupuuza juhudi zao.”
Kauli hiyo imeongeza uzito wa mjadala unaoendelea, huku ikizua maswali mapya kuhusu maadili, uadilifu na nafasi ya wachezaji katika kulinda haki ndani ya mchezo.
Mustakabali wa AFCON uko hatarini?
Wachambuzi wa soka wanaonya kuwa hatua ya Guinea inaweza kuwa mwanzo wa wimbi jipya la mataifa kuhoji matokeo ya zamani, jambo ambalo linaweza kuathiri taswira na historia ya AFCON.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, baadhi wanaona huu ni wakati muafaka kwa CAF kujitathmini na kuweka misingi imara ya haki, uwazi na uwajibikaji.
Kwa sasa, macho ya wadau wa soka barani Afrika yanaelekezwa kwa CAF, ikisubiriwa kutoa msimamo wake uamuzi ambao unaweza kuandika upya historia au kuifunga kabisa sura hiyo yenye utata.
Hivi karibuni, kamati ya Rufaa ya CAF iliipa Morocco ushindi wa mabao 3-0 na kuitangaza kuwa bingwa wa AFCON 2025 kwa madai kuwa Senegal ilifanya kosa la kikanuni katika mchezo wa fainali ambao iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kosa hilo ni la kugomea mchezo ambalo kwa mujibu wa kanuni ya 84 ya mashindano hayo, adhabu yake ni timu pinzani kupata ushindi wa mabao 3-0.