Gamondi awaacha watatu Yanga, Aucho ndani

Muktasari:
- Kikosi cha Yanga kimeondoka jijini Dar es Salaam leo kuifuata Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara huku mastaa watatu wakiachwa.
Dar es Salaam. Timu ya Yanga ipo njiani ikielekea mkoani Kagera kuwafuata Kagera Sugar, lakini msafara wao ukawaacha nyuma mastaa watatu huku Khalid Aucho akirejea.
Kikosi cha Yanga kilichoondoka alfajiri leo Februari mosi, 2024 kikipitia Mwanza kabla ya kuunganisha kwenda Bukoba kimeondoka na msafara wa wachezaji 20.
Kwenye msafara huo, Yanga imewaacha mabeki wake wawili wa kati-- nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad 'Bacca'.
Yanga imelazimika kuwaacha mabeki hao baada ya kupimwa na kugundulika kuwa na majeraha madogo na kulazimika kuwaacha ili wapone sawasawa.
Kocha Miguel Gamondi amesema mabeki hao wataendelea na matibabu, huku akiamini kikosi wanachokwenda nacho kitaweza kupigania pointi tatu.
Mbali na mabeki hao, Yanga pia imemuacha kiungo wake mpya mshambuliaji Augustine Okrah ambaye naye bado hajafanikiwa kuwa sawa sawa baada ya kutoka majeruhi.
"Tungeweza kwenda nao, lakini ni vyema wakapona sawasawa, wachezaji tunaondoka nao tunaamini wataweza kupigania ushindi wa timu yetu,"amesema Gamondi.
Yanga itakutana na Kagera Sugar kesho saa 10 jioni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba mkoani humo.
Hata hivyo, habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kwamba kiungo wao Khalid Aucho amerejea kazini baada ya kumaliza adhabu yake ya kusimamishwa mechi tatu.
Aucho alikumbana na rungu hilo la Bodi ya Ligi Tanzania baada ya kubainika kumpiga kiwiko beki wa Coastal Union wakati timu hizo zilipokutana Uwanja wa Mkwakwani, Yanga ilishinda kwa bao 1-0.
Wachezaji 20 waliondoka ni pamoja na makipa Aboutwalib Mshery, Metacha Mnata, mabeki wakiwa Yao Attohoula, Lomalisa Mutambala, Dickson Job, Gift Fred, Nickson Kibabage na Kibwana Shomari.
Wamo viungo Zawadi Mauya, Pacome Zouzoua, Jonas Mkude, Maxi Nzengeli, Farid Mussa, Aucho, Salum Abubakar 'Sure boy', Mahalatse Makudubela 'Skudu', Shekhan Khamis huku washambuliaji wakiwa Joseph Guede, Kennedy Musonda na Clement Mzize.