Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni dakika 90 za heshima Afrika

Dar es Salaam. Yanga iko kwenye vita ya dakika 90 za kusaka heshima itakapokutana na Medeama ya Ghana katika mchezo wa tatu kwa timu zote kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Baba Yara huko Kumasi, mji unaokadiriwa kuwa na watu milioni 3.3 kwa mujibu wa sensa yao ya mwaka 2020, utaanza saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Mabingwa hao wa Tanzania akili yao kwenye mchezo huo ni moja tu kubwa kusaka ushindi wao wa kwanza kwenye hatua hii wakikumbuka kwamba walishapoteza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria kisha kulazimisha sare nyumbani dhidi ya bingwa mtetezi Al Ahly ya Misri.

Ushindi kwa Yanga leo utaamsha matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.

Yanga ambayo ilitua nchini humo mapema siku tatu kabla kwa ajili ya mchezo huo,  jana ilifanya mazoezi yake ya mwisho huku kila kitu kikionekana kwenda sawasawa kambini kwenye hoteli ya kisasa ya Ridge Condos.

Habari njema kwa Yanga ni kutua kwa staa wao Stephanie Aziz KI ambaye mara baada ya mchezo wa Al Ahly alitimka nchini kwa ruhusa maalum ya kwenda kwao kwa matatizo ya kifamilia na juzi alirudi kundini na kufanya mazoezi na wenzake akionekana yuko sawasawa.


HESABU ZA GAMONDI

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ni kama ameshamaliza kazi yake kwani anajua kila taarifa za wapinzani wake na ameliambia Mwananchi kuwa suala lililosalia ni wachezaji wake kwenda kufanya kweli.

Gamondi licha ya kukiri kwamba mchezo utakuwa mgumu alisema wamejipanga sawasawa kucheza kwa nidhamu na kusaka ushindi dhidi ya Medeama.

“Kwenye mashindano kama haya kila timu unatakiwa ucheze nayo kwa heshima kwa kuwa wote wamestahili kuwa hapa tulipo, tunatakiwa kucheza kwa umakini mkubwa hii ni timu ambayo ina wachezaji bora wenye mbinu,” alisema Gamondi.

“Tunajua namna wanavyocheza wakiwa nyumbani nafikiri kila kitu tumeshamaliza kwa wachezaji tusubiri kuona kipi kitatokea, karibu wachezaji wote tuliokuja nao wako sawasawa.”


AHADI NONO

Nje ya uwanja tajiri wa Yanga, Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ na uongozi wa klabu hiyo wameicheza mechi hiyo kwa akili wakiwapa ahadi nzito ambayo ni sawa na ile waliyowapa timu ilipocheza dhidi ya Simba na Al Ahly.

Mwananchi linafahamu kwamba endapo Yanga itashinda, kila goli la mchezo huo litanunuliwa kwa Sh 100 milioni na idadi ya mwisho ya mabao hayo kutakuwa na ziada ya Sh 200 milioni.

Ahadi kama hii imewahi kuiponza Simba ilipochapwa mabao 5-1 lakini Al Ahly ilinusurika kwenye mtego huo ikiwanyima fedha ndefu wachezaji wa Yanga ambao hawakuambulia kitu kwenye sare ya bao 1-1.

Hata hivyo, Yanga inafahamu kwamba malengo yao hayo hayataweza kutimia kirahisi kwani Medeama sio timu rahisi ikiwa nyumbani, rekodi zikionyesha kwenye mechi zake tatu za nyuma za ligi ya mabingwa imeshinda zote dhidi ya Remo Stars (1-0), Horoya AC (3-1) na Belouizdad (2-1).

Yanga pia itakumbuka kwamba mara ya mwisho ilipokutana na Medeama nchini humo Julai 26, 2016 kwenye mchezo wa makundi wa marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua kama hii walikubali kichapo cha mabao 3-1 baada ya awali kulazimishwa sare ya bao 1-1 hapa nchini.

Msimu huu Medeama ina kitu cha hatari ambacho lazima Yanga ijipange nacho kwani katika mechi zao mbili za makundi imekuwa na mabadiliko manne kutoika kikosi kilichocheza dhidi ya Al Ahly waliyopoteza kwa mabao 3-0 na kile kilichokuja kushinda nyumbani dhidi ya Belouizdad.

Yanga itatakiwa kuwa makini na mshambuliaji Jonathan Sowah ambaye alikosekana kwenye mchezo uliopita, taarifa zikionyesha jamaa anajua kufunga mabao ya aina zote.

Sowah aliikosa mechi ya nyumbani dhidi ya Belouizdad kwa kufikisha kadi tatu za njano baada ya kupata kadi ya tatu kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Al Ahly.


MABEKI HAWACHEKANI

Sio ukuta wa Yanga wala Medeama wote una rekodi sawasawa ambapo katika mechi zao mbili zilizopita kila timu imeruhusu mabao manne jambo ambalo zitahitaji kujipanga sawasawa.

 Kocha wa Medeama, Evance Adotey ameliambia Mwananchi kwamba licha ya kushinda mechi ya pili nyumbani, kikosi chake kitaingia kwa tahadhari kubwa kikijua Yanga sio timu rahisi.

Adotey alisema wamejipanga kushinda mechi yao ya pili nyumbani lakini hilo litategemea kama wachezaji wake watazingatia kwa kiwango gani kucheza kwa nidhamu.

“Tunakwenda kukutasna na timu bora, mimi sio mtu wa kupenda kuangalia matokeo ya mechi zilizopita, kitu nilichowaambia wachezaji wangu hatutakiwi kuwadharau Yanga hata kama haijapata ushindi mpaka sasa,” alisema Adotey.

Upande wa Simba inayonolewa na kocha Abdelhak Benchikha yenyewe tayari ipo nchini Morocco  katika mji wa Marrakech tangu jana na tayari kwa mchezo wao wa tatu wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wydad Casablanca utakaochezwa kesho Jumamosi.