Gamondi anavayowapa mtihani mawinga Yanga

Dar es Salaam. Yanga imerejea mazoezini Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar itakayopigwa Desemba 16.
Lakini ni wazi mawinga (viungo wa pembeni) wa timu hiyo kazi wanayo msimu huu chini ya kocha Miguel Gamondi kwani ameonekana hana kipaumbele upande huo.
Tangu atue na kuanza kazi mwanzoni mwa msimu, Gamondi ame kuwa muumini wa viungo wa kati kuliko mawinga jambo linalowapa tabu mawinga kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho na muda mwingi kusota benchi.
Mawinga asilia ndani ya Yanga ni watano ambao ni Jesus Moloko, Farid Mussa, Denis Nkane, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’, na Maxi Nzengeli ambaye amebadilishiwa majukumu na kuwa kiungo mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji.
Gamondi ni muumini wa mfumo wa 4-2-3-1 ambao mara nyingi umekuwa ukihusisha viungo watano na wakati mwingine mifumo ya 5-1-2-2, na 3-5-2, ambayo huwa na viungo wengi wa kati.
Hali hiyo imemfanya kumbadilishia majukumu halisi Maxi na kumtumia kama kiungo mshambuliaji akicheza maeneo sawa na Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki ambao hubadilika wakati mpira ukichezwa uwanjani.
Maxi amecheza mechi zote za Yanga kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika akitumika dakika 1284.
Akizungumzia suala hilo, winga wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ alisema ni jukumu la mawinga waliopo kupambana kumshawishi kocha awapange.
“Kila kocha anataka kutumia wachezaji walio tayari. Nadhani anaowapanga kwa sasa anaona ndio watamfaa, hivyo mawinga wa Yanga waongeze juhudi na wakifanya vizuri mazoezini sidhani kama ataacha kuwapa nafasi kwenye mechi,” alisema SMG.
Mifumo na falsafa za Gamondi imekuwa dozi chungu kwa Moloko, Nkane, Skudu na Farid ambao msimu uliopita walikuwa wakicheza mara kwa mara lakini sasa ni nadra sana kuwaona.
Katika takwimu ilizonazo Mwananchi, Yanga imecheza mechi 16 ikiwa za Ligi Kuu ni tisa na saba za Ligi ya Mabingwa Afrika sawa na dakika 1620, lakini Skudu, Moloko, Nkane na Farid hakuna hata mmoja aliyecheza walau robo ya dakika hizo kwani Moloko ndiye kacheza nyingi kati yao dakika 323.
Katika mechi tisa za ligi Moloko amecheza nne akianza kikosini dhidi ya KMC na kutolewa dakika ya 79, dhidi ya JKT hakucheza, dhidi ya Namungo aliingia akitokea benchi na kucheza dakika 23 na Ihefu aliyocheza dakika 68 huku akikosa nne mfululizo dhidi ya Geita, Azam, Singida na Simba na kuibukia Coastal alipocheza dakika 21 huku akiwa na pasi za mabao mbili.
Mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imecheza saba ikianza na Asas ugenini ambapo Moloko hakucheza lakini ile ya marudiano alicheza dakika 46, zikafuata mbili na El Merrikh ya Sudan ambapo mchezo wa kwanza alicheza dakika moja na wa pili dakika 76.
Nyota huyu ambaye alikuwa na uhakika kikosini msimu uliopita, msimu huu hatua ya makundi hadi sasa amecheza mechi moja dhidi ya CR Belouizdad kwa dakika tisa. Upande wa Farid ambaye msimu uliopita alikuwa na uhakika kucheza, mbele ya Gamondi mambo yamembadilikia kwani kwenye ligi hadi sasa amecheza mechi moja dhidi ya KMC alipoingia dakika 26 za mwisho ilhali kwenye zile saba za kimataifa hajacheza hata dakika moja licha ya kumudu pia kucheza kama beki wa kushoto.
Nkane kwenye ligi amecheza michezo mitatu kati ya tisa. Aliingia dakika za jioni dhidi ya KMC dakika 11 za mwisho, dhidi ya JKT akacheza dakika 12 na Geita Gold dakika 17 huku kimataifa ni dakika 44 katika mechi ya marudiano dhidi ya Asas.
Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alisema kila kocha ana falsafa zake na kinachofanyika sasa ni uamuzi wa Gamondi. “Kwa Gamondi mambo yamebadilika, ana watu wake wachache anaowaamini na mechi nyingi wanacheza wale wale na mfumo ni mmoja ambao hauwapi nafasi mawinga kwani anatumia zaidi viungo,” alisema.
Upande wa Skudu aliyesajiliwa Yanga msimu huu akitokea Marumo Gallants ya Afrika Kusini, mambo ni magumu kwani amecheza mechi tatu kwenye ligi akianza dhidi ya Ihefu kwa dakika 57, kisha dakika 18 mbele ya Singida Fountain Gate na moja dhidi ya Simba. Kimataifa Skudu amecheza dakika 14 kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Wl Merrikh.
Baada ya mechi iliyopita kimataifa dhidi ya Medeama kumalizika, Gamondi aliulizwa swali kuhusu mabadiliko ya wachezaji kikosini na kujibu kwa ufupi tu; “Ni uamuzi wangu.”