FIFA yazipiga rungu Nigeria, DR Congo
Muktasari:
- DR Congo watakutana na mshindi wa mechi kati ya Jamaica na New Caledonia ambapo mechi ya mwisho itaamua tiketi moja kati ya zilizobaki za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limetoa adhabu kali kwa Nigeria na DR Congo kutokana na matukio ya utovu wa nidhamu yaliyotokea katika mechi ya mchujo wa kuwania kufuzu kombe la Dunia 2026 baina ya timu hizo Novemba 16, 2025.
Katika taarifa yake ya hivi karibuni, FIFA imesema timu za nchi hizo zilikiuka baadhi ya vifungu vya kanuni zake za nidhamu kutokana na tabia ya mashabiki wakati wa fainali ya mchujo kwa bara la Afrika ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia Afrika, mechi ambayo DR Congo ilishinda kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bila kufungana.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, mashabiki wa Nigeria walirusha vitu uwanjani wakati wa mchezo, kitendo ambacho FIFA ilisema kilikiuka Kifungu cha 17 na Kifungu cha 17.2.b cha kanuni zake za nidhamu. Kutokana na hilo, Nigeria imetozwa kiasi cha Faranga 1,000 za Switzerland (Sh3.2 milioni)
Shirikisho la Mpira wa Miguu la DR Congo limepokea adhabu kubwa zaidi baada ya FIFA kuamua kwamba mashabiki wao walitumia vielekezi vya mwanga (laser pointers) wakati wa mechi, kosa linalokiuka Kifungu cha 17.2.d cha kanuni hiyo. Hivyo basi, shirikisho hilo limetozwa faini ya Faranga za Switzerland 5,000 za Uswisi (Sh17 milioni).
FIFA imeibainisha kwamba kila uamuzi ulitolewa kulingana na sifa na mazingira maalum ya kila kesi, na ikaongeza kuwa maamuzi hayo bado yanaweza kukatiwa rufaa.
Hata hivyo, muhtasari huo wa nidhamu haukutaja chochote kuhusu malalamiko ya Nigeria kuhusu madai ya DR Congo kutumia wachezaji wasiostahili kucheza, suala ambalo inadaiwa kuwa Nigeria iliibua baada ya mechi.
Shirikisho la Nigeria lilikuwa limewasilisha malalamiko rasmi kwa FIFA likilishutumu shirikisho la DR Congo kwa udanganyifu katika kuruhusu baadhi ya wachezaji kuchezea timu ya taifa licha ya kuwepo kwa maswali kuhusu uraia wao.
Pia lilidai kwamba baadhi ya wachezaji hao “waliosajiliwa kwa udanganyifu” walicheza katika mechi ya mtoano.
Hadi sasa, FIFA bado haijatoa uamuzi kuhusu malalamiko hayo. Wakati huo huo, DR Congo tayari wametangaza kikosi chao kwa ajili ya mechi za mtoano za kimabara zitakazochezwa baadaye mwezi huu.
DR Congo watakutana na mshindi wa mechi kati ya Jamaica na New Caledonia ambapo mechi ya mwisho itaamua tiketi moja kati ya zilizobaki za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026.