Everton yajitosa kwa Grealish

Muktasari:
- Habari hii imekuja siku chache tu baada ya kuripotiwa kuwa Jack Grealish hatakuwa sehemu ya kikosi cha Manchester City kitakachoshiriki Kombe la Dunia la Klabu.
Liverpool, England. Everton imejiunga rasmi katika kinyang’anyiro cha kumsajili nyota wa Manchester City, Jack Grealish, ambaye anatarajiwa kuondoka Etihad majira haya ya joto. Kwa mujibu wa Daily Mail, klabu hiyo ya Merseyside inafuatilia kwa karibu hali ya Grealish, ingawa bado hakuna mazungumzo rasmi yaliyofanyika kati ya pande hizo mbili.
Ripoti kutoka Inside Sport zinasema kwamba, Everton wanavutiwa na uwezekano wa kufanya dili la mkopo, ikizingatiwa kuwa mshahara mkubwa wa Grealish ni 285,000 dola sawa na shilingi 752 milioni anazolipwa kwa wiki ni kikwazo kwa vilabu vingi kutokana na kanuni za Ligi Kuu England kuhusu faida na uendelevu wa kifedha.

Licha ya changamoto hizo, usajili wa Grealish unatazamwa kama tukio kubwa kwa wamiliki wapya wa klabu hiyo The Friedkin Group, ambao wanataka kuleta sura mpya ndani ya klabu kuelekea msimu wao wa kwanza katika uwanja mpya wa Bramley-Moore Dock.
Mbali na nia ya wamiliki hao kuvutiwa na nyota huyo, kocha David Moyes pia amewahi kumuelezea Grealish kama mchezaji bora kabisa wa EPL alipokuwa akitamba na Aston Villa mwaka 2021, Moyes alinukuliwa akisema:

"Yeye ni mchezaji mzuri sana na huenda ni bora zaidi katika Premier League kwa wakati huu. Amefanya kazi kubwa sana katika klabu hiyo (Aston Villa) na kwa sasa ni mmoja wa wachezaji bora zaidi katika ligi."
Kwa sasa, Everton wanaangalia namna ya kuweza kumudu gharama za dili hilo, huku pia wakijua wazi kwamba hawako peke yao katika mbio hizo. Tayari kuna vilabu vingi vya ndani na nje ya Uingereza vinavyohitaji huduma za Grealish, hivyo ushindani unatarajiwa kuwa mkali.
Habari hii imekuja siku chache tu baada ya kuripotiwa kuwa Jack Grealish hatakuwa sehemu ya kikosi cha Manchester City kitakachoshiriki Kombe la Dunia la Klabu linalokuja. Badala yake, nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 na wawakilishi wake wataruhusiwa kuendelea kutafuta timu mpya ambayo itampa nafasi zaidi ya kucheza msimu ujao.

Kocha mpya wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, pia alizungumza wiki hii kuhusu hali ya Grealish, akisisitiza kuwa:
“Ni mchezaji wa kipekee lakini anahitaji dakika nyingi za kucheza. Na kwa sasa hapati hizo dakika. Anahitaji kujitengenezea nafasi kwa kucheza mechi.”
Hii inaonyesha kuwa Grealish analazimika kufanya maamuzi ya haraka kuhusu mustakabali wake ili kuhakikisha anapata nafasi ya kuwa kwenye kikosi cha England kitakachoshiriki Kombe la Dunia mwaka ujao.
Kwa Everton, kumpata Grealish kutakuwa si tu hatua ya kiufundi, bali pia ni ujumbe kwa mashabiki na wapinzani kuwa klabu hiyo imeanza ukurasa mpya wa ushindani katika EPL