Kepa anasubiri kutambulishwa tu Arsenal

Muktasari:
- Kepa Arrizabalaga ameitumikia Chelsea kwa miaka saba tangu alipojiunga nayo 2018 akitokea Athletic Bilbao.
Arsenal inakaribia kumnasa kipa Kepa Arrizabalaga wa Chelsea kwa dau la Pauni 5 milioni ikitegemea awe msaidizi wa David Raya.
Timu hiyo inayonolewa na Arteta imekoshwa na utayari ambao Kepa ameuonyesha wa kushindania nafasi na Raya ambaye ametwaa mara mbili mfululizo tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu England.
Uhamisho huo wa Kepa utafanya kipa namba mbili wa Arsenal hivi sasa, Neto kurejea Bournemouth baada ya kumaliza mkopo wake ndani ya timu hiyo ya London.
Mwaka 2018, Arrizabalaga aliweka rekodi ya kuwa kipa ghali zaidi duniani baada ya kununuliwa kwa ada ya Pauni 71.8 milioni kutoka Athletic Bilbao.
Katika dirisha la majira ya kiangazi 2024, kipa huyo alisaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea Chelsea lakini akapelekwa kwa mkopo Bournemouth.
Msimu uliomalizika wa 2024/2025, Kepa alidaka idadi ya mechi 31 za Ligi Kuu England (EPL) na kuiwezesha timu hiyo kumaliza katika nafasi ya tisa katika msimamo.
Kepa ameonekana kutokuwa chaguo la kocha Enzo Maresca ambaye anawategemea zaidi makipa Filip Jorgensen na Robert Sanchez.
Kepa anakumbukwa kwa kushiriki kuipa Chelsea mafanikio ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2020/2021, Kombe la Europa League 2018/2019, taji la Super Cup 2021 na Klabu Bingwa ya Dunia 2021.