Dube, Azam ngoma mbichi

Dar es Salaam. Wakati Azam FC ikithibitisha kupokea maombi ya kuvunja mkataba ya Prince Dube, mshambuliaji huyo inadaiwa ameendelea kushikilia msimamo wa kutaka kuondoka huku akiripotiwa kuwa tayari kulipa fedha ili aununue mkataba na kuuvunja.
Juzi jioni, ofisa habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema klabu hiyo imepokea barua ya kuomba kuvunja mkataba kutoka kwa Dube na imempa uhuru wa kufanya hivyo ikiwa atalipa kiasi cha fedha ambacho inahitaji.
“Azam Football Club inathibitisha kwamba imepokea barua kutoka kwa Prince Dube, akiomba kuvunja mkataba na klabu yake ambayo ameitumikia tangu 2020. Dube amewasilisha barua kwa uongozi na uongozi umemjibu kama ifuatavyo.
“Kwanza kataba wa Dube ambao alisaini mwishoni mwa msimu uliopita unatakiwa kumuweka Azam FC hadi 2026 kwa hiyo hadi sasa bado ana miaka miwili na nusu. Kwa hiyo klabu imemjibu kwamba kama anataka kuondoka kama ambavyo amewasilisha ombi lake, haina kipingamizi hata kidogo, inamruhusu kuondoka lakini kwa mahitaji ya mkataba kwamba lazima mkataba utekelezwe.
“Kwa hiyo ameambiwa kama anataka kuondoka, atekeleze mkataba kwa kulipa kiasi ambacho kimetajwa kwenye mkataba ambacho ni Dola za Kimarekani 300,000, mkataba ambao ulisainiwa kabla ya kuanza kwa msimu huu lakini amepewa ‘option’ (chaguo) ya pili kwamba kama anadhani kuna klabu inamtaka, ije kufanya maongezi na Azam Fc lakini kwa masharti hayo kwamba gharama yake ya kumnunua ni Dola 300,000 lakini kama hizo mbili zikishindikana, ya tatu ni kuendelea kuwepo hadi mkataba wake utakapoisha aondoke,” alisema Zaka Zakazi.
Baada ya kauli hiyo ya Azam FC, inaripotiwa kuwa jana Dube alikuwa tayari kuilipa Azam FC kiasi cha Dola 200,000 akiamini kingeweza kushawishi uongozi wa timu hiyo ili umfungulie milango ya kuondoka.
Kiasi hicho cha fedha anachotaka kulipa ni kile ambacho Azam walimlipa mwaka jana wakati akaongeza mkataba huo mpya unaomalizika mwaka 2026.
Habari za ndani ya Azam ni kwamba bado kuna majadiliano yanaendelea kuhusiana na dau hilo pamoja na uamuzi wa mchezaji huyo huku wengine wakikereka kwanini amefanya jambo hilo wakati huu?
Wengi wao wanaona kama kaonyesha dharau kubwa na hakuna kingine zaidi ya kumruhusu aondoke ingawa ishu ya dau alilokuja nalo mezani bado halijafikiwa muafaka wowote mpaka muda huu.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema Dube anatarajiwa kujiunga na timu hiyo wiki ijayo na kwamba, mchezaji huyo ana mkataba nao hadi mwaka 2026.
Hadi sasa Dube amecheza dakika 734 kati ya dakika 1710 za mechi 19 za Azam FC msimu huu. Dakika alizocheza ni katika mechi 12, huku akikosa mechi saba kati ya mechi 19.
Kwa kifupi ni kwamba Dube amecheza chini ya nusu ya dakika za jumla kama angecheza mechi zote msimu huu na hii ni kutokana na pancha za hapa na pale ambazo kimsingi zimekuwa zikimuandama katika misimu yote.
Katika dakika hizo 734 za mechi 12 ambazo amecheza, amefunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao.
Mkataba wa Dube na Azam FC unatarajiwa kumalizika ifikapo Juni 2026, ikiwa na maana kwamba bado ana misimu miwili na nusu mbele.