Dewji ajivua uenyekiti Bodi ya Simba, Magori apewa kijiti
Muktasari:
- Bodi ya Simba inaundwa na Wajumbe 16 ambapo Wajumbe nane ni kutoka upande wa Wanachama na Wajumbe nane kutoka upande wa mwekezaji.
Dar es Salaam. Mwaka mmoja baada ya kuongoza Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Bilionea Mohammed Dewji amejiondoa katika nafasi hiyo na kumteua Crecentius Magori.
Dewji ambaye ni mwekezaji wa klabu hiyo ametangaza uamuzi huo leo Septemba 4, 2025 huku akitaja sababu kuwa ni kubanwa na majukumu yake binafsi.
“Kwa muda mrefu nimekuwa nikihudumu kama Rais wa Simba SC na Mwenyekiti wa Bodi. Hata hivyo, kutokana na majukumu yangu mengine na ukweli kwamba mara nyingi nipo mbali, nimeona ni muhimu klabu yetu ipate kiongozi wa bodi ambaye yupo karibu, mwenye muda wa kutosha na anaweza kushiriki kwa ukaribu zaidi katika shughuli za kila siku.
“Kwa msingi huo, ninatangaza rasmi kwamba nitaendelea kubaki kama Mwekezaji na Rais wa Simba SC, lakini nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi sasa inakabidhiwa kwa kiongozi mpya.
“Ningependa pia kutumia nafasi hii kuwashukuru kwa dhati wajumbe wote wa bodi waliotangulia kwa vongozi wao, muda na chango wao mkubwa katika maendeleo ya Simba SC. Kila mmoja wenu ameacha alama ya kipekee katika safari ya klabu yetu,” amesema Dewji.
Dewji amesema kuwa nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu hiyo kwa sasa itachukuliwa na Crescentius Magori.
“Kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Kampuni (MEMARTS) ya Simba Sports Club Company Limited, Ibara ya 41, Rais anatokana na MO Simba Company Ltd na anayo mamlaka ya kufanya uteuzi wa viongozi wa Bodi.
“Kwa mamlaka hayo, nimeamua kumteua Ndugu Crescentius Magori kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba SC,” amesema Dewji.
Dewji pia ametangaza uteuzi wa Wajumbe saba wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba ambao wanatoka upande wake kama mwekezaji.
Wajumbe hao ni Barbara Gonzalez, Hussein Kitta, Azim Dewji, Rashid Shangazi, Swedi Mkwabi, Zuly Chandoo na George Ruhango.