Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mo Dewji achomoza tena orodha ya matajiri Afrika

Muktasari:

  • Utajiri wa Mo Dewji wapaa, ashika nafasi ya 12 Afrika.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohammed Dewji (Mo) ametajwa na Jarida la Forbes kuwa tajiri namba 12 barani Afrika, na bilionea kijana zaidi kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.

Kwa mujibu wa jarida hilo mashuhuru ambalo hufuatilia ukwasi wa watu, ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita Mo amepanda kwa utajiri barani Afrika kutoka nafasi ya 15 hadi 12.

Mfanyabiashara huyo anayemiliki Kampuni ya Mohammed Enterprises Ltd (METL), utajiri wake umepanda kutoka Dola bilioni 1.5 za Marekani (Sh3.77 trilioni) mwaka uliopita hadi Dola bilioni 1.8 (Sh4.52 trilioni), jambo linalomfanya kuwa tajiri namba moja ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Ripoti inaonyesha kwa ujumla ukwasi wa mabilionea 20 wanaoongoza Afrika uliongezeka kwa Dola milioni 900 (Sh2.26 trilioni) na kufika Dola bilioni 82.4 (Sh207.23 trilioni) mwaka 2024.

Upimaji wa ukwasi wa watu uliofanywa na Forbes uliangalia gharama halisi kwenye masoko ya mitaji na viwango vya kubadilishia fedha vilivyopo sokoni hadi Januari 8, 2024.

METL ambayo imejikita kwenye biashara mbalimbali zikiwamo za vyakula na vinywaji, ikimiliki viwanda kadhaa ndani na nje ya Tanzania, imeajiri zaidi ya wafanyakazi 40,000.

Katika orodha hiyo, bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote aliyejikita kwenye viwanda vikiwamo vya saruji anashika nafasi ya kwanza akiwa na utajiri wa Dola bilioni 13.9 bilioni za Marekani akifuatiwa na Johann Rupert, nafasi ya pili akiwa na utajiri wa Dola bilioni 10.1 za Marekani.

Nafasi ya tatu inashikwa na familia ya Nicky Oppenheimer yenye utajiri wa Dola bilioni 9.4, huku Nassef Sawiris akishika nafasi ya nne akiwa na utajiri wa Dola bilioni 9.4. Sehemu kubwa ya utajiri wa Nassef unatokana na uwekezaji kwenye biashara ya madini.  

Mwingine aliye kwenye orodha ya mabilionea 20 barani Afrika ni Mike Adenuga mwenye utajiri wa Dola bilioni 6.9 akishika nafasi ya tano, huku Abdulsamad Rabiu akishika nafasi ya sita akiwa na utajiri wa Dola bilioni 5.9.

Naguib Sawiris, aliyejikita kwenye biashara ya mawasiliano anashika nafasi ya saba akiwa na utajiri wa Dola bilioni 3.8. Mohamed Mansour anashika nafasi ya nane akiwa na utajiri wa Dola bilioni 3.2 bilioni. Tajiri namba tisa kwa mujibu wa Forbes ni Koos Bekker, anayejikita kwenye biashara za mawasiliano na burudani akiwa na utajiri wa Dola bilioni 2.7. 

Bilionea wa Afrika Kusini, Patrice Motsepe anashika nafasi ya tisa akiwa na utajiri wa Dola bilioni 2.7. Bilionea huyu ambaye amejikita kwenye biashara za madini, pia ni mmiliki wa klabu ya Mamelod Sundown ya Afrika Kusini.

Motsepe kwa sasa ndiye Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) akiwa amefanya uwekezaji mkubwa kwenye soka nchini Afrika Kusini.

Nafasi ya 11 kwenye orodha hiyo inashikiliwa na Familia ya Issad Rebrab akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola bilioni 2.5 akiwekeza zaidi kwenye biashara ya vyakula na vinywaji.

Mfanyabiashara na mwekezaji kwenye klabu ya Simba, Mohammed Dewji (Mo) anashika nafasi ya 12 kwenye orodha ya mabilionea barani Afrika akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.8 bilioni. Kwa sasa ni Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba.

Katika kampuni za METL, licha ya kuajiri Watanzania wengi, Mo pia amekuwa sehemu ya msaada kwa jamii kupitia Taasisi ya Mo Foundation iliyojikita kusaidia vijana wa Kitanzania kutimiza ndoto zao kielimu.

Mo Foundation imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo kila mwaka kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kusoma vyuo vya ndani na nje ya Tanzania.

Katika orodha hiyo, Strive Masiyiwa anashika nafasi ya 13 akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.8, Aziz Akhannouch anashika nafasi ya 14 akiwa na Dola bilioni 1.7.

Nafasi ya 15 inashikiliwa na Othman Benjelloun akiwa na Dola bilioni 1.4, Youssef Mansour anashika nafasi ya 16 akiwa na Dola bilioni 1.3, Yasseen Mansour yuko nafasi ya 17 akiwa na ukwasi wa Dola bilioni 1.2, huku Christoffel Wiese akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.2 katika nafasi ya 18.

Wengine ni Michiel Le Roux katika nafasi ya 19 akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.1 na Femi Otedola anafunga dimba la 20 bora akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.1.