Dabi ya Kariakoo kupigwa Meja Jenerali Isamuhyo
Muktasari:
- Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Dabi ya Kariakoo kupigwa katika dimba hilo ambalo linabeba idadi ya mashabiki 15000.
Dar es Salaam. Baada ya siku kadhaa za sintofahamu, Wekundu wa Msimbazi, Simba wameweka nukta.
Klabu hiyo imethibitisha kuwa mechi ya mzunguko wa pili ya Ligi Kuu Bara ya 'Dabi ya Kariakoo’ dhidi ya Yanga itachezwa katika Dimba la Meja Jenerali Isamuhyo, Mei 3, 2026.
Simba, ambao watakuwa wenyeji wa mechi hiyo wameamua kuendelea kutumia uwanja huo ambao umekuwa ngome yao kwa sasa, huku mashabiki wakisubiri kuona kama Isamuhyo itatoa mbabe baada ya suluhu kule Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.
Simba inakwenda kukutana na Yanga ambao ndio vinara wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 47 mbele ya Wekundu hao ambao wanashika nafasi ya pili kwa pointi 42 huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 19.
Katika michezo mitano ya mwisho ya Ligi Kuu ambayo wamekutana, Yanga ndio wababe wa dabi hiyo kubwa Afrika Mashariki wakiwa wameshinda mara nne na kutoa sare mechi moja.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Dabi ya Kariakoo kupigwa katika dimba hilo ambalo linabeba idadi ya mashabiki 15000.
Timu zote zipo Zanzibar kwa sasa zikishiriki Michuano ya Muungano ambapo kesho Yanga itacheza hatua ya nusu fainali dhidi ya Azam na Jumapili Simba ikivaana na Mlandege.